Abu Turabi Fard: Marekani ndiyo sababu ya ukosefu wa usalama duniani, si Iran
(last modified Fri, 16 May 2025 10:25:37 GMT )
May 16, 2025 10:25 UTC
  • Abu Turabi Fard: Marekani ndiyo sababu ya ukosefu wa usalama duniani, si Iran

Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya hapa Tehran amesema: "Katika hali ambayo Israel inafanya mauaji ya kutisha zaidi kwa niaba ya Marekani, inazikalia kwa mabavu nchi za Kiislamu, na kukanyaga haki ya kujitawala kitaifa Lebanon, Syria na Yemen, rais wa Marekani anadai kiuongo kuwa eti Iran ndiyo tishio kwa usalama wa eneo, wakati ni Marekani ndiye tishio."

Hujjatul Islam Sayyid Mohammad Hassan Abu Torabi Fard, amesema hayo katika khutba za Sala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran na huku akigusia safari ya hivi sasa ya rais wa Marekani Donald Trump ya kuzitembelea nchi za Kiarabu za eneo hili amesema kuwa, Trump amekuja kwenye eneo hili kwa lengo la kuficha uhalifu wa Marekani na Israel, kufanya biashara na kuutafutia fedha utawala wa Kizayuni na wakati huohuo anafanya upotoshaji wa makusudi wakati ukweli uko wazi.

Amesema: "Katika wakati ambao Israel imeonesha nusu ya sura yake ya giza na ya kikatili, imefanya mauaji ya kutisha zaidi kwa niaba ya Marekani na madola ya Magharibi, inafanya vitendo vya kigaidi, na kukanyaga haki ya kujitawala nchi za Lebanon, Syria na Yemen, Trump anajipa uthubutu wa kudai hadharani kwamba eti Iran ni tishio la usalama wa eneo hili.

Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amebainisha pia kwamba, tangu Agosti 19, 1953 hadi leo, katika kipindi cha miongo saba, Marekani haijasita kufanya uovu wowote wa kutishia usalama wa Iran na wa eneo hili zima na muda wote imekuwa ikifanya njama za kuzuia maendeleo na ustawi wa Iran. Marekani ilimchochea na kumuunga mkono Saddam, muda wote imeiwekea vikwazo vikali zaidi Iran, inakiuka haki za binadamu za taifa hili na uhalifu mwingine mwingi wa serikali mbalimbali za Marekani. Lakini amesema, ana imani mshikamano wa Umma wa Kiislamu, utalinda maslahi ya umma huo mbele ya njama za maadui.