Katibu Mkuu wa UN: Maendeleo ya kidijitali yanawaacha nyuma wanawake
(last modified Sun, 18 May 2025 04:19:49 GMT )
May 18, 2025 04:19 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN: Maendeleo ya kidijitali yanawaacha nyuma wanawake

Tarehe 17 Mei 2025, Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (TEHAMA), ulimwengu umeadhimisha miaka 160 tangu kuanzishwa kwa Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano, ITU, kwa kuangazia mchango wa teknolojia katika kubadilisha maisha ya binadamu kuanzia kwenye telegrafu hadi redio, kutoka mtandao wa intaneti hadi akili mnemba AI.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, katika ujumbe wake wa siku hii ametoa wito wa kuhakikisha mabadiliko ya kidijitali yanakuwa ya usawa wa kijinsia.

Ametahadharisha kuwa licha ya maendeleo makubwa kiteknolojia, faida zake bado zinapatikana kwa njia isiyo na usawa.

“Upendeleo wa kihisia unaosababisha ubaguzi katika algorithmi unadumaza usawa. Ukatili na udhalilishaji wa mtandaoni unanyamazisha sauti za wanawake na kuwafanya wajitenge na mifumo ya kidijitali,” amesema Katibu Mkuu.

Aidha Guterres ameelezea wasiwasi kuhusu uwakilishi mdogo wa wanawake na wasichana katika taaluma za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) maeneo ambayo yanaathiri moja kwa moja mwelekeo wa maendeleo ya baadaye.

“Uonevu unatuumiza sote. Hatupaswi kuukubali mustakabali wa kidijitali unaowaacha wanawake nyuma. Tunapaswa kuwekeza katika stadi za kidijitali kwa wote, kutumia teknolojia kuboresha maisha ya wanawake, kuondoa vizuizi vinavyowazuia kushiriki kikamilifu na kuongoza katika sekta ya teknolojia, na kuendelea kupambana na ukatili wa kijinsia mtandaoni na nje ya mtandao,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, mikataba mipya kama "Mkataba wa Zama Zijazo" na "Mkataba wa kimataifa wa dijitali" ni fursa muhimu ya kuunganisha nguvu duniani kote ili kufunga pengo la kidijitali na kulinda haki za wanawake katika majukwaa ya kidijitali.

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza kuwa “Wakati teknolojia inapotumika kwa manufaa ya wote, kila mtu hunufaika." 

Wakati huo huo, Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Iran amesema kuwa lengo kuu la wizara yake ni kuifanya Iran kuwa kitovu cha kuunganisha “uchumi wa kidijitali” katika ukanda huu wa kijiografia.

Akizungumza katika maadhimisho ya “Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ” yaliyofanyika Tehran siku ya Jumamosi, Sattar Hashemi alieleza kuwa takribani dola za Kimarekani bilioni 25 hadi 30 zinahitajika ili Iran iweze kufikia angalau asilimia 10 ya uchumi wa kidijitali katika pato la taifa (GDP).

Ameongeza kuwa uwekezaji wa jumla uliofanywa na waendeshaji wa huduma za mawasiliano nchini mwaka uliopita (uliomalizika Machi 20, 2025) ulikuwa chini ya dola bilioni 2.