Iran yataka maendeleo ya Akili Mnemba katika nchi za Kiislamu
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Mohammad-Reza Aref, ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kuwekeza na kuendeleza Akili Mnemba (AI) kwa kuzingatia kanuni kuu tatu za ushirikiano wa pande kadhaa, mshikamano wa kisayansi, na miundombinu ya pamoja.
Aref ameongeza kuwa, “Kwa hiyo, ninawasilisha mapendekezo maalum kwa ajili ya maendeleo na kuhamasisha ushirikiano kati ya nchi za Kiislamu katika sekta ya sayansi na teknolojia, hasa Akili Mnemba.”
Alitoa kauli hiyo Jumatatu alipokuwa akihutubia Mkutano wa Pili wa Mawaziri wa Jukwaa la Mazungumzo la Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC-15).
Pendekezo la kwanza linaangazia umuhimu wa kuanzishwa kwa kikundi cha juu kinachoongoza maendeleo ya Akili Mnemba katika kundi hilo la OIC-15, lengo likiwa kuunda mfumo wa kufuatilia maendeleo ya dunia katika nyanja ya Akili Mnemba.
Pendekezo la pili linahusu kuandaa ramani ya njia ya muda wa kati na muda mrefu kwa ajili ya ushirikiano wa kisayansi na kiteknolojia katika Akili Mnemba.
Pendekezo la tatu linasisitiza kuunganisha vyuo vikuu na vituo vya utafiti ili kutumia na kushiriki ujuzi na uwezo wa wataalamu na taasisi mbalimbali duniani ya Kiislamu kwa ajili ya utafiti na maendeleo ya pamoja, kushirikiana katika kuendeleza teknolojia, na kuanzisha programu za pamoja za kitaaluma kuhusu Akili Mnemba.
Pendekezo la nne linaelekeza ufadhili wa pamoja wa utafiti wa Akili Mnemba, miradi ya kiteknolojia, na miundombinu ili kusaidia miundombinu muhimu, miradi ya kimkakati ya pamoja, na kuanzisha kampuni changa za Akili Mnemba zinazotumia uwezo wa nchi za Kiislamu, pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu.
Na pendekezo la mwisho limesisitiza kuandaa mkataba wa Kiislamu kuhusu maadili ya Akili Mnemba ili kuunda mfumo wa ndani unaotegemea misingi ya sheria ya Kiislamu, heshima ya binadamu, na haki za kijamii.
Mkutano wa Pili wa Mawaziri wa Jukwaa la Mazungumzo la OIC-15 ulifanyika kuanzia Mei 17 hadi 19.
Kaulimbiu ya mkutano wa siku tatu ilikuwa juu ya Akili Mnemba chini ya anuani ya “Ubunifu katika Sayansi na Teknolojia kwa Kutumia Akili Mnemba: Mkakati wa Ubora, Maisha Bora kwa Ulimwengu wa Kiislamu.”
Mkutano huu ulitumiwa kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia kuimarisha diplomasia ya kisayansi. Pia ulikuwa fursa ya kupitia na kujadili changamoto za nchi za Kiislamu katika sekta ya teknolojia.
Mkutano ulilenga hasa Akili Mnemba katika elimu ya juu, ukizungumzia changamoto na fursa, pamoja na athari za Akili Mnemba katika maendeleo ya kiuchumi. Aidha, waraka wa kwanza wa pamoja wa pande nyingi kuhusu Akili Mnemba kati ya nchi za Kiislamu ulitarajiwa kuidhinishwa wakati wa mkutano huu.