Awamu ya tano ya mazungumzo ya Iran na Marekani kufanyika kesho Ijumaa
(last modified Thu, 22 May 2025 06:08:09 GMT )
May 22, 2025 06:08 UTC
  • Awamu ya tano ya mazungumzo ya Iran na Marekani kufanyika kesho Ijumaa

Esmail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, duru ya tano ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani itafanyika kesho Ijumaa nchini Italia.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran iliyotolewa usiku wa kuamkia leo imemnukuu Baqaei akizungumzia pendekezo lililotolewa na Oman na mashauriano yake ya kufanyika duru nyingine ya mazungumzo ya Iran na Marekani siku ya Ijumaa katika mji mkuu wa Italia, Rome na kutangaza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imekubaliana na pendekezo hilo.

Amesema: Timu ya mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nia safi na imesimama kidete katika kutafuta haki na maslahi ya juu ya taifa la Iran yaani kunufaika na nishati ya nyuklia ya matumizi amani, ikiwa ni pamoja na kurutubisha urani na kuondolewa vikwazo vya kidhalimu, hivyo haitoacha kufanya juhudi na kuunga mkono mpango wowote utakaofanikisha suala hilo.

Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikuwa amesema kuwa, Tehran bado haijaamua iwapo itashiriki katika duru ijayo ya mazungumzo ya nyuklia au la. Sayyid Abbas Araghchi alisisitiza kwamba urutubishaji wa madini ya urani utaendelea ndani ya Iran iwe ni kwa kufikiwa makubaliano au bila ya makubaliano yoyote.

Msimamo huo wa Iran unathibitisha msisitizo wake wa kulinda haki zake kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), hasa kurutubisha madini ya urani na kuondolewa vikwazo.