Jeshi la Anga la Iran liko imara kuilinda nchi kwa nguvu zote
(last modified Mon, 02 Jun 2025 02:58:32 GMT )
Jun 02, 2025 02:58 UTC
  • Jeshi la Anga la Iran liko imara kuilinda nchi kwa nguvu zote

Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIAF), Brigedia Jenerali Hamid Vahedi amesema kuwa, jeshi hilo liko imara na limejiandaa kikamilifu kulinda anga ya Jamhuri ya Kiislamu kwa hali yoyote ile.

Kamanda Vahedi ameyasema hayo katika mkutano wake na makamanda wa Jeshi la Wanahewa wa kituo cha anga cha Shahid Habibi kilichoko Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran, jana Jumapili.

Amesema kuwa, majibu ya haraka ni miongoni mwa msingi muhimu zaidi wa Jeshi la Anga la Iran hasa kwa kuzingatia hali tete iliyopo katika eneo hili hivi sasa.

Ameongeza kuwa, kikosi chake lazima kidumishe utayari wake endelevu na kuimarisha uwezo wake muda wote.

"IRIAF iko tayari kutoa ulinzi madhubuti wa anga ya nchi yetu (Iran) kwa hali yoyote ile," amesema Brigedia Jenerali Vahedi.

Vilevile amesisitizia umuhimu wa kutumiwa maarifa asilia katika Jeshi la Anga na kusema: "Tuna wajibu wa kudumisha uwezo wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kiwango cha juu zaidi kwa kutegemea utaalamu na maarifa ya ndani."

Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilevile amesema kuwa, jeshi hilo ndio mstari wa mbele wa kukabiliana haraka na tishio lolote dhidi ya nchi.

Kama inavyobainsha miongozo ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, viongozi mbalimbali wa Iran nao muda wote wamekuwa wakisisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu haitosita kuimarisha uwezo wake wa kijeshi, ambao ni kwa ajili ya kujihami pekee na kwamba suala hilo si kitu cha kujadiliwa kabisa.