Eslami: Urutubishaji wa madini ya urani ni mstari mwekundu kwa Iran
Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki la Iran (AEOI), Mohammad Eslami, amesema kwa msisitizo kuwa urutubishaji wa madini ya urani ni jambo la msingi lisilojadiliwa katika sera za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akilitaja kuwa ni "mstari mwekundu" kwa taifa.
Katika mahojiano yaliyotangazwa kupitia runinga na kuchapishwa Jumatatu, Eslami amesema: “Urutubishaji wa urani ndiyo msingi na nguzo kuu ya sekta ya nyuklia ya Iran. Ni mstari mwekundu kwa Jamhuri ya Kiislamu.”
Ameendelea kusisitiza kuwa Iran haitakubali kubanwa wala kuzuiwa kuendeleza teknolojia hiyo. Amesema: “Hakuna anayeweza kuiambia Iran kwamba haina haki ya kurutubisha madini ya urani. Hili ni jambo la ndani ya taifa letu, lenye mfumo na mahitaji maalum.”
Kauli hiyo imekuja kufuatia mashinikizo kutoka kwa Marekani, utawala wa Israel, mshirika wa karibu wa Washington katika eneo la Asia Magharibi, na baadhi ya madola ya Magharibi, ambayo yamekuwa yakitaka Iran ipunguze kiwango chake cha urutubishaji wa urani hadi kufikia sifuri.
Marekani imesisitiza msimamo huo mara kadhaa, ikiwemo katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Tehran yaliyoanza mwezi Aprili. Licha ya hayo, viongozi wa Iran wameendelea kushikilia msimamo wao bila kuyumba.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, pia amesisitiza kuwa urutubishaji wa madini ya urani ni sehemu muhimu ya shughuli za nyuklia za amani za Iran. Ameongeza kuwa Iran itaendeleza shughuli hizo kwa mujibu wa sheria zake, yawepo makubaliano na Marekani au la.
Katika mahojiano hayo, Eslami pia amezungumzia ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) kuhusu shughuli za nyuklia za Iran, akieleza kutoridhishwa na kile alichokitaja kuwa ni ripoti ya kisiasa iliyoandaliwa kwa ushawishi wa mataifa ya Magharibi na utawala haramu wa Israel.

Amesema: “Ripoti hiyo imeandaliwa kwa mtazamo wa sera ileile ya ‘mashinikizo ya juu kabisa’ yanayoongozwa na Marekani kwa kushirikiana na washirika wake.”
Eslami amewataja waliokuwa nyuma ya mashinikizo hayo kwa IAEA kuwa ni Marekani na mataifa matatu ya Ulaya , Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, ambao ni washirika wa karibu wa Washington barani Ulaya.
Kwa mujibu wake, mashinikizo hayo yalitokana na ushawishi wa kile alichokiita “utawala wa Kizayuni wa Israel,” na kwamba kwa sababu ya mashinikizo hayo, shirika hilo limetoa ripoti “iliyojaa tuhuma na mada zilezile ambazo tayari zimepatiwa majibu.”
Amefafanua kuwa kila mara Shirika la IAEA linapowasilisha ripoti kwa Bodi ya Magavana, Iran huichambua kwa kina na kuwasilisha majibu yenye maelezo ya kisayansi na kisheria ili kupinga hoja zilizoibuliwa.