Iran yaishtaki IAEA kwa madai yake yasiyo na msingi
(last modified Fri, 06 Jun 2025 06:47:46 GMT )
Jun 06, 2025 06:47 UTC
  • Iran yaishtaki IAEA kwa madai yake yasiyo na msingi

Iran imetoa hati ya kisheria kupinga madai ya “ujasusi” ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kuyataja kuwa ni ya kichochezi na yasiyo na msingi. Tehran inaamini kuwa shirika hilo limevuka mipaka yake na linatoa matamshi dhidi ya Iran kwa kutegemea ushahidi bandia.

Kwa mujibu wa hati ya kisheria iliyosambazwa kati ya wanadiplomasia siku chache kabla ya mkutano muhimu mjini Vienna; Iran imezidisha msimamo wake dhidi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia kwa kuwashutumu wakaguzi wa shirika hilo kwa kufanya kashfa ya kuwasilisha ushahidi wa uongo usio na msingi wowote.

Kanali ya televisheni ya Bloomberg News imetangaza kuwa: "Memo hiyo inaonyesha kwamba mvutano kati ya Tehran na IAEA umeongezeka kabla ya mkutano wa Juni 9.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mvutano kati ya Iran na IAEA umekuja wakati ambapo mazungumzo kati ya Iran na Marekani yamekumbwa na kizuizi kutokana na Marekani kushikilia msimamo wake wa kuinyima Iran haki yake ya kisheria na ya kimataifa ya kurutubisha madini ya urani.

Katika uchambuzi wa kwanza wa kina wa ripoti ya ukaguzi wa IAEA tarehe 31 Mei, Iran ilimshutumu Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi kwa kupotosha shughuli za nyuklia za Iran kwa kutoa taarifa za uwongo na zinazojirudiarudia.

“Shirika la IAEA limeikasirisha Iran kwa matamshi ya uongo ya mkurugenzi wake Rafael Grossi” imeongeza taarifa hiyo.

Wakaguzi wa IAEA wanaendelea kutembelea maeneo ya nyuklia ya Iran kila siku na watakuwa na jukumu muhimu katika uhakiki ikiwa makubaliano yatafikiwa kati ya Iran na Marekani.

Iran imeandika katika barua iliyosambazwa kwa wanachama wa IAEA kwamba: "Iwapo nchi za Magharibi zitaamua kutumia vibaya subira ya Iran na kuendelea na chokochoko zao, basi Tehran italazimika kuchukua na kutekeleza maamuzi yanayofaa kwa mujibu wa hatua zitakazochukuliwa na upande wa pili.

Kabla ya hapo, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisisitiza kwamba "ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki zinapaswa kuwa za kiufundi na zisiwe za kisiasa."