Pezeshkian: Iran kamwe haitokubali kuwa chini ya ubeberu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran daima inakaribisha mazungumzo na maneno ya kimantiki, lakini kamwe haiko tayari kuwa chini ya ubeberu wa mtu yeyote yule.
Rais Masoud Pezeshkian amsema hayo wakati alipoonana na Murat Nurtleu, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje ya Kazakhstan hapa Tehran na huku akigusia mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani amesema: Visingizio visivyo na msingi kuhusu mradi wa amani wa nyuklia wa Iran vinatolewa katika hali ambayo, Tehran imesema mara chungu nzima kuwa, kamwe haina nia ya kumiliki silaha za nyuklia na imeonesha kivitendo kuwa silaha za mauaji ya umati zikiwemo za nyuklia hazina nafasi yoyote katika mikakati ya kiulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Rais Pezeshkian amesisitiza kwamba shughuli za nyuklia za Iran ziko wazi kikamilifu na hilo limethibitishwa kwenye ripoti chungu nzima za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA. Ameongeza kuwa, Iran haijakataa kufanyiwa ukaguzi mradi wake a nyuklia lakini itaendelea kusimama imara kulinda haki yake katika teknolojia hiyo na haikubaliki kuyanyima mataifa ya dunia, elimu, teknoojia na mafanikio ya kisayansi ya nishati hiyo muhimu. Amesema, teknolojia ya nyuklia ni muhimu sana katika sekta za tiba, kilimo na uvumbuzi mbalimbali wa kisayansi, hivyo kuyanyima mataifa ya dunia teknolojia ya nyuklia ni kuwanyima waja wa Mwenyezi Mungu neema kubwa.
Kwa upande wake, Murat Nurtleu, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje ya Kazakhstan ameelezea furaha yake kwa kupata nafasi ya kuonana ana kwa ana na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa nchi yake inaheshimu misimamo imara na ya kimantiki ya Iran.