Mngurumo wa mwisho wa Israel: 'Simba Anayeinukia' kusambaratishwa na kimbunga cha Iran
Mashambulio ya utawala ghasibu wa Israel katika miji kadhaa ya Iran yamefanyika leo alfajiri huku mivutano na hali ya wasi wasi ikiendelea kuongezeka katika eneo, jambo linaloonyesha wazi nia ya Tel Aviv ya kuchochea machafuko katika eneo hili tata la Asia Magharibi, ambapo anga inabadilika haraka kwa maslahi ya mrengo wa muqawama.
Iran, ikiwa tayari imeonyesha uwezo wake wa makombora na ndege zisizo na rubani katika makabiliano ya huko nyuma, sasa iko katika nafasi nzuri zaidi ya kutoa majibu makali na ya kuumiza na hivyo kufafanua upya uwiano wa nguvu katika eneo. Ripoti za awali za mashambulizi hayo ziliripotiwa katika mji mkuu Tehran, na kufuatiwa na msururu wa milipuko katika mikoa mingine kadhaa. Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha uharibifu mkubwa uliosababishwa na mashambulio hayo katika makazi ya raia, na hivyo kuonyesha kuwa maeneo yote ya kiraia na kijeshi yalijumuishwa kwenye mashambulo hayo. Israel baadaye ilitoa taarifa ikitangaza kuhusika na mashambulizi hayo katika maeneo ya Natanz, Khorramabad, Khondab na maeneo mengine. Jeshi la Israel limeiita operesheni hiyo kuwa ‘Simba Anayeinukia’.
Kitendo cha uchokozi huu usiohalalishwa kwa njia yoyote ile, kimetekelezwa huku matamshi ya chuki na uchochezi yakitolewa na watawala Israel, wakiongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambaye sera zake za kuchochea vita zinaendelea kuyumbisha eneo hili. Huku Marco Rubio Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akijaribu kuiweka mbali Washington na mashambulizi hayo, na kuyaita "hatua ya upande mmoja," wajuzi wa mambo ya eneo wanaamini kwamba operesheni hiyo kubwa isingeweza kutekelezwa bila ya kuwepo kwa uchache uungaji mkono wa kimyakimya wa Marekani, hasa katikati ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington.
Mbali na uharibifu uliofanywa kwenye majengo na miundo msingi ya Iran, shambulio la Israel limeua shahidi wanajeshi kadhaa wa Iran. Iran imeahidi kutoa jibu kali, na kuweka wazi kwamba chokochoko hizo hazitapita bila kujibiwa.
Mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel katika ardhi ya Iran ni katika msururu wa uchokozi wake wa wazi dhidi ya nchi za eneo kwa ushirikiano wa karibu na Marekani. Mnamo Aprili 1, mwaka uliopita, ndege za kivita za Israel ziliwaua washauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria, washauri ambao walitumwa huko kwa ombi rasmi la rais wa zamani wa Syria Bashar al-Assad ili kusaidia kupambana na makundi ya kigaidi yakiongozwa na Daesh. Katika kujibu uchokozi huo, Iran ilishambulia kwa ndege zisizo na rubani na makombora zaidi ya 300 shabaha za kijeshi za Israel kupitia "Operesheni ya Ahadi ya Kweli."

Operesheni hiyo ilipata mafanikio makubwa ya kimkakati. Kama ilivyoripotiwa na gazeti la The New York Times, "Baada ya kubainika kuwa Iran ingelipiza kisasi, maafisa wa Marekani na Israel walidhani kuwa kiwango cha jibu kingekuwa kidogo, lakini baada ya kubainika hasara iliyosababishwa na jibu hilo kali walitafunatafuna maneno wakijaribu kuhalalisha kilichotokea na kujaribu kufunika uharibifu uliosababishwa na mashambulizi hayo. Mashambuli hayo bila shaka yaliweka wazi nguvu ya Iran ya kuzuia mashambulizi ya adui na vilevile kushindwa kwa vyombo vya ujasusi vya Israel.
Wakati huo, Brigedia Jenerali Zvika Haimovich, kamanda wa zamani wa ulinzi wa anga wa Israel, alikiri kwamba Iran sasa ni "nguvu kuu katika makombora ya kimbinu ya balestiki na ndege zisizo na rubani." Chas Freeman, mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani, aliunga mkono maoni hayo, akisema: “Inaonekana kwamba katika kambi kubwa ya kijeshi huko kusini, ambako walilenga, waliweza kufikia kiwango cha usahihi ambacho kilikuwa cha kushangaza sana.” Freeman aliongeza, "Iran ilifanikiwa kuwatia hofu wakazi wa Israel .... inaweza kulemaza ulinzi wa Israel ikiamua kufanya hivyo, na wala Israel haiwezi kujilinda bila msaada mkubwa wa Marekani, Uingereza, Ufaransa na pia Jordan."
Kisha "Operesheni ya Ahadi ya Kweli II" iliyofanywa mwezi Oktoba mwaka uliopita ilithibitisha zaidi uwezo wake unaoendelea kukua. Katika kujibu mauaji ya viongozi wa mrengo wa muqawama, akiwemo Ismail Haniyeh wa Hamas, Sayyed Hassan Nasrullah wa Hezbollah na Abbas Nilforoushan, kamanda wa jeshi la IRGC, Iran ilirusha makombora 200 katika vituo muhimu vya kijeshi na kijasusi vya Israel. Kila shambulio lilituma ujumbe wa wazi: "Tehran haitavumilia tena uchokozi usiodhibitiwa."
Operesheni za Ahadi ya Kweli za I na II zilitikisa misingi ya fikra za kimkakati za utawala ghasibu wa Israel. Operesheni hizi zilianika peupe udhaifu wa Israel na kuvunjilia mbali ngano isiyo na msingi ya muda mrefu kuwa Israel haiwezi kushindwa kijeshi.
Kufuatia uchokozi wake wa Ijumaa alfajiri, Israel kwa mara nyingine tena imeikasirisha nguvu ya kieneo ambayo tayari imeonyesha kuwa inaweza kupiga kwa usahihi mkubwa maeneo ya kistratijia ya utawala huo. Azma ya Iran haijawahi kuwa wazi zaidi, bila shaka itajibu tu uchokozi huo, sio lazima iwe ni kwa haraka, bali la kuumiza na kwa wakati unaofaa. Kila jibu linamaanisha kuwa uwiano wa kijeshi unabadilika kwa madhara ya Israel.
Israel, katika ukiukaji wake wa mara kwa mara wa sheria za kimataifa na kutojali maisha ya raia, inachezea moto. Kadiri muqawama unavyoongezeka na miungano ya kikanda kuimarika, Israel inajikuta ikitengwa zaidi katika eneo.