Araghchi: Iran ‘imejiandaa kikamilifu’ iwapo Israel itavunja usitishaji vita ‘dhaifu’
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128514
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema Jamhuri ya Kiislamu iko macho na iko tayari kujilinda iwapo utawala wa Israel utavunja usitishaji vita "tete" uliohitimisha siku 12 za uchokozi wa utawala huo wa Kizayuni dhidi ya nchi hii mwezi uliopita.
(last modified 2025-07-19T14:37:25+00:00 )
Jul 19, 2025 14:25 UTC
  • Araghchi: Iran ‘imejiandaa kikamilifu’ iwapo Israel itavunja usitishaji vita ‘dhaifu’

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema Jamhuri ya Kiislamu iko macho na iko tayari kujilinda iwapo utawala wa Israel utavunja usitishaji vita "tete" uliohitimisha siku 12 za uchokozi wa utawala huo wa Kizayuni dhidi ya nchi hii mwezi uliopita.

Sayyid Araghchi aliyasema hayo katika mahojiano na Televisheni ya Kimataifa ya China (CGTN) mjini Tianjin, China, ambako alikuwa ameenda kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO) siku ya Jumanne.

Amebainisha kuwa, vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala wa Israel dhidi ya Iran vilikuwa ni uchokozi wa kijeshi, na wala sio tu "mgogoro." "Sio mzozo. Ni kitendo cha uchokozi, uchokozi wa makusudi wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," amesisitiza.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amebainisha kuwa, "Hatukuwa na njia ila kutekeleza haki yetu ya kujilinda. Kwa hivyo, tuliilinda nchi yetu. Tuliilinda kwa ujasiri mkubwa na tukawalazimu wavamizi kuacha uchokozi na kuomba usitishaji vita bila masharti, ambao tuliukubali,"

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran vile vile ametilia shaka nia ya Israel ya kuheshimu kweli na ka dhati usitishaji huo wa mapigano, ambao ameutaja kama "dhaifu".

"Usitishaji vita, bila shaka, ni dhaifu na sababu ni dhahiri: hakuna usitishaji vita wa utawala (wa Israel) unaotegemewa kwa sababu utawala huo una rekodi mbaya sana juu ya hilo," ameelezea Raghchi.

Amesisitiza kuwa, "Tuko makini sana na tumejitayarisha kikamilifu ikiwa usitishwaji wa mapigano utavunjwa, lakini haya sio matakwa yetu. Hiyo haikuwa azma yetu tangu mwanzo. Hatukutaka vita hivi, lakini tulikuwa tayari kwa hilo."