Iran yatilia shaka 'hadhi' ya Tuzo ya Nobel baada ya Trump 'kuteuliwa'
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baqaei ametilia shaka itibari na uhalisi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, akisema tuzo hiyo yenye heshima kubwa zaidi ya amani duniani, imegeuzwa na kuwa chombo cha kisiasa badala ya kuwa nembo ya amani kwa wote.
Wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari hapa Tehran, Baqaei alijibu swali kuhusu uteuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa tuzo hiyo mwaka huu, akiliita "Maskini Nobel, Maskini Amani."
Amesisitiza kuwa, tuzo za amani kama vile Nobel haziwezi kupewa "itibari" sana, haswa zinapogeuzwa wahanga wa siasa, ubaguzi, na upotoshaji wa ukweli.
"Katika ulimwengu wa haki na bora, mmoja wa wagombea wanaostahiki zaidi Tuzo ya Amani ya Nobel bila shaka ni Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu," Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema.
Ameongeza kuwa, Albanese, licha ya mashinikizo na vitisho, anaendelea kutetea haki za Wapalestina wanaodhulumiwa. "Leo, tunaishi katika ulimwengu ambao sio tu hauna haki, lakini umepitia aina ya ubadilishaji wa thamani," ameongeza.
Huu ni ulimwengu ambapo, "Tuzo ya Amani ya Nobel inang'aa kwa majina kama Nelson Mandela - kutokana na mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi wa apartheid (nchini Afrika Kusini)- lakini sasa tuko katika zama ambapo nembo za apartheid na ubaguzi wa rangi, na wale wanaofanya mauaji ya kimbari na uvamizi, wanajiweka katika nafasi ya kuteua wengine kwa tuzo hii," Baqaei amesema.
Alikuwa akimzungumzia Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ambaye alimteua Trump kwa Tuzo ya Nobel, mkabala wa uungaji mkono wake kwa utawala huo, alipoitembelea Washington mapema mwezi huu.
Kabla ya hapo, Mkuu wa zamani wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alikemea pendekezo la Netanyahu la kutaka Trump atunukiwe Tuzo ya Amani ya Nobel, akilielezea hilo kuwa ni hatua iliyochukuliwa na "mtu anayeaminika kuwa mhalifu wa kivita" kwa ajili ya "muuzaji wake mkuu wa silaha".