Baqaei: Iran haiwezi kuiamini Marekani baada ya kushambulia vituo vyake vya nyuklia
-
Esmail Baqaei
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa nchi hii haiiamini Marekani khasa baada ya mashambulizi yake yasiyo na msingi katika vituo vya nyuklia vya Iran vinavyoendesha shughuli zake kwa malengo ya amani.
Akizungumza na televisheni ya Press ya Iran, Esmail Baqaei amesema, katika vita vya siku 12 vilivyoanzisha na utawala ghasibu wa Israel, Washington ilishirikiana na Israel kukiuka mamlaka ya kujitawala Iran na kuhujumu juhudi za kidiplomasia ziliozokuwa zikiendelea.
Israel ilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Iran tarehe 13 Juni mwaka huu na kuwauwa shahidi makamanda kadhaa wa jeshi wa ngazi ya juu, wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida.
Wiki moja baadaye, Marekani pia iliingia katika vita hivyo kwa kushambulia vituo vitatu vya nyuklia nchini Iran vinavyoendesha shughuli zao kwa malengo ya kiraia.
Israel na Marekani zilianzisha vita hivyo katikati ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington kuhusu miradi ya nyuklia ya Tehran.
"Hakuna mpango wa kufanya mazungumzo ya aina yoyote na Marekani, lakini mara zote tumekuwa tukisema kwamba Iran kamwe haijawahi kuondoka kwenye meza ya mazungumzo," amesema Esmail Baqaei.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameweka wazi kuwa: Iwapo tutaelewana kwamba tunaweza kupata ufumbuzi wa jambo kupitia mazungumzo au tunaweza kutetea maslahi yetu ya kitaifa hatutasita kufanya hivyo.
Ameongeza kuwa mazungumzo yanapasa kuwa na madhumuni na yenye mwelekeo wa kupata ufumbuzi na si kuinyima Iran haki zake stahiki kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).