IRGC: Taifa liko tayari kuvunja safu yoyote ya adui
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesisitiza kuwa taifa la Iran liko tayari kusimama kidete kukabiliana na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu na kuwalazimisha wasalimu amri kama lilivyofanya katika makabiliano yaliyopita.
Jeshi la IRGC limetoa matamshi hayo kupitia taarifa iliyotolewa leo Jumapili, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kurejea nchini wafungwa waliokombolewa katika vita vilivyolazimishwa dhidi ya Iran na dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein katika miaka ya 1980.
IRGC imewataja wafungwa hao waliokombolewa kama "nembo ya kweli ya muqawama hai na matumaini ya kimkakati."
IRGC imesisitiza kwamba ushindi wa askari hao wa zamani dhidi ya adui katika ushindi mpana wa taifa wakati wa vita vya miaka minane uliakisiwa tena katika kuzima uchokozi wa Israel na Marekani dhidi ya Iran mwezi Juni uliopita.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilikuwa likiashiria tukio la hivi karibuni ambapo utawala wa Israel ulilazimika kuomba usitishaji vita Juni 24, licha ya kupata msaada mkubwa wa kijeshi na kifedha usio na mfano wake kutoka Marekani na nchi nyingine za Magharibi katika muda wote wa uchokozi wa siku 12 dhidi ya Iran.
Jeshi hilo limeongeza kuwa, moyo huo huo wa ushindi unadhihirika katika nguvu za muqawama wa Palestina na kushindwa mara kwa mara kwa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi.
Kikosi hicho kimewapongeza wanajeshi hao wa zamani kuhusu azma yao thabiti ambayo ilithibitisha kwamba "nguvu ya imani, umoja wa kitaifa, na uthabiti wa kimapinduzi vinaweza kulazimisha mashine kubwa zaidi za vita na sera za kibeberu kupiga magoti."