Iran: Tutatumia zana mpya iwapo adui ataanzisha tena uchokozi
Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh amesisitiza kuwa, iwapo maadui watafanya uchokozi mwingine dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, bila shaka majeshi ya nchi hii yatatumia vifaa, silaha na zana za kijeshi ambazo hazijawahi kutumiwa kufikia sasa.
Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh alisema hayo wakati wa mahojiano maalum ya televisheni jana Ijumaa na kubainisha kuwa, "Ikiwa adui atafanya uchokozi mwingine, bila shaka tutapeleka vifaa ambavyo bado havijawahi kutumiwa."
Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh amelitaja kombora la 'Qasem Basir' la nchi hii kuwa moja ya makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ambayo hayakuvurumishwa katika kipindi chote cha operesheni za kujihami kutakatifu na kulipiza kisasi, ambazo zilifanyika katika kukabiliana na vita visivyo na msingi vya utawala wa Israel na Marekani mwezi Juni.
Amelielezea kombora hilo - linaloweza kupiga umbali wa kilomita 1,200 (maili 745) - kuwa kombora la maangamizi na lenye usahihi wa hali ya juu la Iran.
"Kombora hilo limetengenezwa kwa kutumia utaalamu wa kiteknolojia ambao ulitokana na operesheni ya kulipiza kisasi ya Ahadi ya Kweli I na II dhidi ya vitendo vya uchokozi vya Israel mwaka jana," ameeleza kamanda huyo na kuongeza kuwa, "Ujuzi uliotumika kutengeneza kombora hilo umelifanya liwe na uwezo wa kukabili bila kusita vita vya kielektroniki vya adui, na hatua za kukabiliana na sumakuumeme."
Wakati huo huo, Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu Iran Meja Jenerali Amir Hatami amesisitiza kuwa Vikosi vya Ulinzi vimejiweka tayari kutoa jibu kwa wavamizi ambalo ni la "kusagasaga zaidi" kuliko lile lililoonekana wakati wa uchokozi uliofanywa na utawala haramu wa kizayuni wa Israel na Marekani dhidi ya taifa hili.
Kadhalika Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea pia utayari wa Majeshi wa "kupiga hatua kubwa zaidi - kwa kutumia uwezo wa kitaifa - ili kufikia vilele vya ustawi na nguvu".