Araghchi: Historia haitasamehe usuasuaji zaidi katika kukomesha janga la Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129986-araghchi_historia_haitasamehe_usuasuaji_zaidi_katika_kukomesha_janga_la_gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ametoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kimataifa kukomesha mauaji ya halaiki ya Israel yanayoendelea huko Gaza, akisema kuwa nchi zote zinapaswa kusimama upande sahihi wa historia ambao "hautasamehe" ucheleweshaji wowote zaidi wa kupunguza mateso ya watu wa Palestina.
(last modified 2025-08-25T11:51:52+00:00 )
Aug 25, 2025 11:50 UTC
  • Araghchi: Historia haitasamehe usuasuaji zaidi katika kukomesha janga la Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ametoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kimataifa kukomesha mauaji ya halaiki ya Israel yanayoendelea huko Gaza, akisema kuwa nchi zote zinapaswa kusimama upande sahihi wa historia ambao "hautasamehe" ucheleweshaji wowote zaidi wa kupunguza mateso ya watu wa Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo leo Jumatatu alipokuwa akiwahutubia mawaziri wenzake katika mji wa Jeddah nchni Saudi Arabia, ambapo walikutana katika mkutano wa dharura juu ya mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Palestina.

"Tukumbuke kuwa maafa ya Gaza hayawahusu Waislamu pekee. Ni mtihani kwa dhamiri ya kimataifa. Kwa hivyo, tunatoa wito kwa mataifa yote, bila kujali dini au jiografia, kusimama upande wa ubinadamu, haki, na heshima, ambayo ni upande sahihi wa historia," amesema Araghchi na kusisitiza kuwa, "Historia haitasamehe usuasuaji. Gaza haiwezi kusubiri. Wakati wa kuchukua hatua ni sasa," ameongeza.

Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC umefanyika kufuatia ombi la Iran, ambalo lilitumwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi kwa Katibu Mkuu wa OIC, mnamo tarehe 6 Agosti.

Sayyid Araghchi ameeleza bayana kuwa: Leo, tumekusanyika wakati ambapo Gaza inasimama mbele ya dhamiri yetu kama kioo kinachoogofya. Kinachojitokeza mbele ya macho yetu ni uharibifu uliopangwa wa watu waliozingirwa, na utawala dhalimu wa ubaguzi wa rangi ambao unafanya unalotaka bila kubebeshwa dhima au kuadhibiwa.

Ameeleza kuwa, watu wa Gaza wanauawa kwa utaratibu maalum, maeneo ya makazi yameharibiwa kabisa; hospitali zimegeuzwa kuwa makaburi; na watoto wamenasa katika njaa kali; huu ukiwa ukiukaji wa wazi wa kila kiwango cha binadamu. Hivi sivyo vita vya kawaida. Ni adhabu ya pamoja, sera ya kutawala, na mashambulio ambayo yana ishara zote za mauaji ya kimbari.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria Hadithi ya Mtume Muhammad (SAW) alipotufundisha kwamba, Umma wa Kiislamu ni kama mwili na roho moja. "Leo, mwili huu una maumivu na umerowa kwa damu huko Gaza. Kukaa kimya ni kujiumiza wenyewe, na hatua ya ujasiri ndiyo njia ya uponyaji," amefafanua mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran.

Hali kadhalika, Waziri Araghchi amezitolea wito nchi za Kiislamu kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na ajenda ya kujitanua ya Israel katika eneo la Asia Magharibi kupitia kampeni ya 'Israel Kubwa Zaidi'.

Ameongeza kuwa, ili kuanzisha mchakato wa amani na kuhakikisha vikosi vamizi vya Israel vinaondoka kikamilifu kutoka kila shibri ya Gaza, lazima tujitolee kuhamasisha utumiaji wa zana zote za kisiasa, kiuchumi na kisheria ikiwa ni pamoja na vikwazo, ususiaji wa bidhaa, na mashinikizo ya kimataifa yaliyoratibiwa.