Qalibaf alaani chokochoko za Marekani dhidi ya Venezuela
Mohammad Qalibaf Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amelaani chokochoko za Marekani katika eneo la Caribbean dhidi ya Venezuela.
Qalibaf amekosoa na kulaani hatua hatari na chokochoko za serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani zinazoilenga Caracas na kuitaja Venezuela kuwa ni rafiki na mshirika wa Iran. " Tunalaani visingizio vya Marekani dhidi ya Venezuela na hatua zake za uchokozi katika eneo la Caribbean," amesema Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran. Mohammad Qalibaf ameeleza haya katika mazungumzo ya simu na Spika wa Bunge la Taifa la Venezuela, Jorge Rodriguez.
Ameongeza kuwa si vita vya siku 12 dhidi ya Iran wala vitisho vya Marekani dhidi ya Venezuela ambavyo vinapasa kuvuruga makubaliano ya pande mbili, na kutilia mkazo kuhusu kushirikiana pakubwa kivitendo kati ya nchi mbii hizi waitifaki.
Spika wa Bunge la Taifa la Venezuela ameishukuru Iran kwa msimamo wake thabiti dhidi ya Israel na kusema: Hatua za Marekani dhidi ya Caracas ni kali za kibeberu na kwamba tuhuma zilizoelekezwa kwa Venezuela kwamba inajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya ni za uwongo.
" Venezuela si mzalishaji wala kituo cha kupitisha dawa za kulevya, katika hali ambayo Marekani inaongoza kwa matumizi ya dawa haramu, huku uchumi wake ukihusishwa na utakatishaji fedha na biashara ya mihadarati," amesema Jorge Rodriguez.