Araqchi: IAEA imeafiki haja ya mfumo mpya wa ushirikiano na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130416-araqchi_iaea_imeafiki_haja_ya_mfumo_mpya_wa_ushirikiano_na_iran
Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa hakutakuwa na ushirikiano mpya baina ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) hadi hapo mazungumzo yatakapokamilika.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 04, 2025 22:49 UTC
  • Sayyid Abbas Araqchi
    Sayyid Abbas Araqchi

Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa hakutakuwa na ushirikiano mpya baina ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) hadi hapo mazungumzo yatakapokamilika.

"Tutafanya kila tuwezalo kuzuia kurejeshwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa na kubainisha kuwa utaratibu wa Snapback ni kinyume cha sheria," ameeleza mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Iran.

Mataifa matatu makubwa ya Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yameitishia Iran kuhusu kutekeleza utaratibu wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi yake. 

Tehran  kwa upande wake inasisitiza kuwa hatua hiyo ya nchi hizo tatu za Ulaya (E3) ni kinyume cha sheria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza haya akijibu matamshi ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambaye ameitaka Iran ikubali haraka iwezekanavyo kukaguliwa maeneo yake ya nyuklia. 

Grossi pia amesema: Wakala wa IAEA utajaribu kufanya mkutano mwingine na Iran siku chache zijazo. 

Tehran tayari imepasisha sheria ya kusimamisha ushirikiano na IAEA . Aidha imeeleza kuwa  Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran linapasa kutoa kibali cha kuruhusu ukaguzi wowote katika siku zijazo na wakala wa IAEA. 

Shirika la habari la Associated Press Jumatano wiki hii liliripoti kuwa Tehran na IAEA hazijafikia makubaliano kuhusu kukaguliwa taasisi za nyuklia za Iran.