Larijani azitaka serikali za Kiislamu kuchukua hatua dhidi ya jinai za Israel
Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran katika ujumbe wake amezitaka serikali za Kiislamu kuchukua hatua madhubuti na za kivitendo dhidi ya jinai za Israel.
Katika ujumbe wake aliotuma katika mtandao wa kijamii wa X akizitahadharisha serikali za Kiislamu, Larijani ameeleza kuwa kitendo cha kuitisha Mkutano waJumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ambao umejaa hotuba bila matokeo yoyote ya kivitendo (kama inavyotokea katika vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa) kiuhalisia ni sawa na kutoa amri mpya ya uvamizi yaani kuunga mkono utawala wa Israel.
"Serikali za Kiislamu kwa uchache anzisheni chumba cha pamoja cha oparesheni dhidi ya uwendawazimu wa utawala huu," ameongeza kusema Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.
Ali Larijani amesema uamuzi huu pekee unatosha kuwatia wasiwasi wakuu wa utawala huo na kuwasukuma haraka kubadili amri zao kwa kisingizio cha kuleta amani ya dunia na Tuzo ya Nobel.
Amezihutubu serikali za Kiislamu akisema kuwa hazikufanya lolote kwa wananchi madhulumu na wanaotabika na njaa wa Palestina. Serikali hizo angalau zichukua uamuzi mdogo ili kuzuia uharibifu dhidi yao.