Juhudi za mhimili wa Magharibi za kuchafua jina la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Wanachama wa Mchakato wa Radiamali ya Haraka wa Kundi la G7 ambazo ni nchi za Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya, pamoja na Australia na New Zealand, katika taarifa ya pamoja siku ya Ijumaa walidai kulaani hatua za Iran kuhusiana na eti kuongezeka kwa kampeni ya ukandamizaji unaotekelezwa nje ya mipaka yake.
Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Australia, Kanada, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, New Zealand, Uingereza na Marekani inadai kuongezeka juhudi za mashirika ya upelelezi na intelijensia ya Iran kwa ajili ya kuchukua hatua dhidi ya wapinzani wa kisiasa nje ya nchi.
Madai ya Wamagharibi kuhusiana na suala hili yanakinzana wazi na hali ya makundi ya upinzani ya Iran yaliyoko nje ya nchi likiwemo kundi la kigaidi la Munafiqeen MKO, ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakijishughulisha na uharibifu na chuki dhidi ya Iran katika nchi za Ulaya na Marekani chini ya msaada na uungaji mkono wa moja kwa moja wa serikali za Magharibi. Ikiwa madai haya kuhusu juhudi za mashirika ya upelelezi ya Iran za kukabiliana na upinzani nje ya nchi ni ya kweli, na kwa kutilia maanani uwezo wa Iran ambao ulidhihirika wazi wakati wa kukabiliana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni, kwa kupiga kwa umakini mkubwa maeneo tofauti ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, kwa kutumia makombora na ndege zake zisizo na rubani, ni wazi kuwa Tehran ina uwezo mkubwa wa kukabiliana vilivyo na makundi hayo ya kigaidi, na ikiwa haichukui hatua yoyote dhidi ya makundi hayo, ni kwa sababu ya nguvu kubwa ya Tehran, ambapo haiyachukulii makundi hayo ya kisaliti kuwa tishio kwa usalama wake wa kitaifa.
Wakati huo huo madai hayo ya uwongo yametolewa na nchi za Magharibi dhidi ya Iran, huku nchi hizo hizo zikiwa zimefumbia macho kwa muda mrefu hatua za kigaidi na kinyama zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina kwa ushirikiano na uungaji mkono wa moja kwa moja wa nchi za Magharibi. Nchi hizo hizo pia zinawaunga mkono kikamilifu wapinzani na makundi ya kigaidi ya Iran ambayo huko nyuma yamefanya mauaji ya umati na kutekeleza ugaidi na ghasia za umwagaji damu ndani ya ardhi ya Iran. Mfano wa wazi wa hilo ni kimya cha Wamagharibi kuhusiana na hatua nyingi za utawala wa Kizayuni za kuwaua kigaidi wapinzani wake katika nchi za nje, ima kwa kutumia magenge ya kigaidi au kwa njia ya mashambulizi ya kushtukiza na hivi karibuni mashambulizi ya anga ambayo yamekuwa yakitekelezwa bila ya kizuizi kwa uungaji mkono kamili wa Marekani. Kimsingi, Wamagharibi daima hutumia siasa za undumakuwili wanapokabiliana na masuala nyeti kama vile ugaidi na ukandamizaji wa ndani, iwe ni ukandamizaji wa wanahabari au jamii za wachache.
Sasa, suala hili linaonekana wazi katika taarifa ya kundi la G7 pamoja na Australia na New Zealand. Swali kuu ni je, ni nini sababu ya Wamagharibi kuwa na hisia kali dhidi ya Iran na kutoa kila aina ya tuhuma bila ya kutoa uthibitisho au ushahidi wa kutosha katika uwanja huo?
Ikiwa tuhuma zinazotolewa na nchi hizo dhidi ya Iran ni mfano wa ukiukwaji wa haki za binadamu na ugaidi unaodhaminiwa na dola, kwa nini nchi hizo hizo zisichukue misimamo inayofaa dhidi ya hatua za uchokozi na ugaidi zinaotekelezwa wazi wazi na Israel kisha utawala huo huo kutangaza hadharani kwa kiburi na majigambo kuhusika na vitendo hivyo?
Kuna mifano mingi ya vitendo vya kigaidi na kichokozi vinavyofanywa na Israel ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na katika nchi nyingine za eneo. Moja ya matukio ya hivi karibuni kuhusu vitendo hivyo vya kigaidi ni shambulizi la anga la Israel dhidi ya makao makuu ya viongozi wa Hamas nchini Qatar, ambalo ni kielelezo tosha cha kutojali utawala huo katika kukiuka mamlaka na ardhi ya Qatar, na pia ukiukaji wa wazi wa sheria na kanuni za kimataifa. Ni wazi kuwa hiyo ni ishara na thibitisho tosha la ugaidi wa kiserikali. Jambo la kuzingatiwa hapa ni kuwa ugaidi na uchokozi huo unafanyika kwa uungaji mkono kamili na wa wazi wa Marekani pamoja na misimamo laini ya ushirikiano wa nchi za Magharibi kwa suala hili.
Bila shaka, nchi hizi za G7 na washirika wao zina historia ndefu ya kuunga mkono tawala kandamizi katika miongo iliyopita. Moja ya mifano ya wazi ni uungaji mkono kamili wa Marekani kwa utawala wa Jenerali Pinochet, dikteta wa zamani wa Chile katika miaka ya 1970, ambaye alichukua madaraka baada ya mapinduzi dhidi ya Salvador Allende, rais wa mrengo wa kushoto wa Chile, na hatimaye kuuawa mwaka 1973. Alikuwa rais wa Chile kwa miaka 17 hadi 1990. Wakati wa utawala wa Pinochet, kulikuwa na ukandamizaji mkubwa dhidi ya uhuru wa kujieleza, waandishi wa habari na upinzani kwa jumla nchini Chile. Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa na tume ya serikali nchini humo mwaka 2011, idadi ya wahanga ambao walifungwa na kuteswa wakati wa utawala wa Pinochet ilifikia 40,000, ambapo watu 3065 walipoteza maisha. Hii ni pamoja na ukweli kwamba Marekani na nchi za Magharibi si tu hazikulaani wala kuukosoa utawala wa Pinochet kwa vitendo hivyo, bali Washington iliendelea kuwa mmoja wa waungaji mkono wakuu wa dikteta huyo wa Chile.