Iran yaonya kuwa itasitisha mkataba wa IAEA iwapo vikwazo vya UN vitarejeshwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131054-iran_yaonya_kuwa_itasitisha_mkataba_wa_iaea_iwapo_vikwazo_vya_un_vitarejeshwa
Mwanadiplomasia mwandamizi wa Iran amesema kuwa makubaliano ya hivi karibuni kati ya Tehran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA yaliyofikiwa mjini Cairo yatasitishwa ikiwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa vitarejeshwa au utaratibu unaoitwa snapback.
(last modified 2025-09-21T03:25:43+00:00 )
Sep 21, 2025 03:25 UTC
  • Iran yaonya kuwa itasitisha mkataba wa IAEA iwapo vikwazo vya UN vitarejeshwa

Mwanadiplomasia mwandamizi wa Iran amesema kuwa makubaliano ya hivi karibuni kati ya Tehran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA yaliyofikiwa mjini Cairo yatasitishwa ikiwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa vitarejeshwa au utaratibu unaoitwa snapback.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi ameyasema hayo katika mahojiano ya simu aliyofanyiwa na IRIB News akijibu hatua ya Ulaya ya kurejesha maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, licha ya ushirikiano mkubwa uliopo baina ya Iran na Troika ya Ulaya na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) katika siku za hivi karibuni.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa lilipiga kura dhidi ya rasimu ya azimio ambalo lingeondoa kabisa vikwazo vinavyohusishwa na mpango wa nyuklia wa Iran.

Gharibabadi amesema, ingawa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kupinga Azimio nambari 2231 na makubaliano ya nyuklia ya JPOA, lakini hatua hiyo ilishindwa kupata kura zinazohitajika.

Wanachama tisa walipinga hatua hiyo, huku Russia, China, Pakistan na Algeria wakiunga mkono, na wanachama wawili walijizuia kupiga kura. Hii ina maana kwamba, vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vitawekwa tena ifikapo Septemba 28 iwapo hakuna makubaliano yatakayofikiwa.

Amesema: "Sisi, China, na Russia tumewasilisha hoja zetu za kina na za kisheria kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika miezi ya hivi karibuni, na wakati wa majadiliano hayo ya kina, tulitangaza kwamba hatua za nchi hizi tatu za Ulaya (Uingereza, Ufaransa na Ujerumani) kuzusha utaratibu wa snapback ni kinyume cha sheria kikamilifu." 

Tarehe 9 mwezi huu wa Septemba, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi walifikia makubaliano juu ya mbinu za kivitendo za kurejesha ushirikiano katika mazungumzo ya ana kwa ana yaliyofanyikaCairo, mji mkuu wa Misri.