Pezeshkian: Iran inatoa kipaumbele kuimarisha uhusiano na China
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran katika ujumbe wake kwa mwenzake wa China, Xi Jinping, amesisitiza kuwa Tehran inatoa kipaumbele kwa suala la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na wa kina na Beijing.
Kwa niaba ya taifa na serikali ya Iran, Rais Pezeshkian ameupongeza uongozi na taifa la China kwa mnasaba wa Siku ya Taifa ya China, akiitaja kuwa ni ishara ya umoja, maendeleo na mafanikio aali ambayo yamechangia ustawi wa dunia.
Akizungumzia mkutano wake wa hivi majuzi na Rais Xi Jinping mjini Beijing, Pezeshkian amesisitiza kuwa, ushirikiano wa kistratajia na China ni kipaumbele kikuu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesisitiza kwamba, mazingira magumu ya sasa ya kimataifa na kikanda yanafanya uimarishaji na upanuzi wa uhusiano wa pande zote kati ya nchi hizo mbili kuwa muhimu zaidi kuliko hapo awali.
Katika ujumbe wake huo kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 76 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, Rais wa Iran amesisitiza kuwa, Siku ya Taifa ya China inaashiria umoja, maendeleo na mafanikio makubwa ya nchi hiyo katika maendeleo yanayochangia pakubwa ustawi wa dunia.
Dakta Pezeshkian amekumbusha kuwa, uhusiano wa kihistoria kati ya Iran na China unarudi nyuma maelfu ya miaka, na kwamba mataifa haya mawili yana ustaarabu wa kale na wenye mizizi imara.
Rais wa Iran ameeleza matumaini yake kwamba, kuheshimiana na maslahi ya pamoja ni mambo ambayo yataimarisha zaidi uhusiano kati ya mataifa haya mawili rafiki.