Pezeshkian: Jenerali Soleimani alikuwa nembo ya maelewano na utiifu kwa Kiongozi Muadhamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135016-pezeshkian_jenerali_soleimani_alikuwa_nembo_ya_maelewano_na_utiifu_kwa_kiongozi_muadhamu
Rais Masoud Pezeshkian amesisitiza kwamba, taifa la Iran litaendeleza njia ya Shahid Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na viongozi wengine wa kambi ya Muqawama akiongeza kuwa, shahidi Soleimani alikuwa nembo ya maelewano, huruma na utiifu kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
(last modified 2026-01-02T02:48:36+00:00 )
Jan 02, 2026 02:48 UTC
  • Pezeshkian: Jenerali Soleimani alikuwa nembo ya maelewano na utiifu kwa Kiongozi Muadhamu

Rais Masoud Pezeshkian amesisitiza kwamba, taifa la Iran litaendeleza njia ya Shahid Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na viongozi wengine wa kambi ya Muqawama akiongeza kuwa, shahidi Soleimani alikuwa nembo ya maelewano, huruma na utiifu kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Rais Pezeshkian alisema hayo jana Alkhamisi, Januari 1, 2026, katika kumbukumbu za kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani zilizofanyika kwenye Mosalla wa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Jenerali Soleimani alikuwa msaidizi mkubwa wa wanyonge, mpigania haki na ukweli na alifanya kazi bila ya upendeleo, bila ya majigambo, na bila ya kutafuta umaarufu na ni kwa sababu hiyo ndio maana amekuwa nembo na mfano wa kuigwa si tu nchini Iran bali pia katika nchi zote za dunia.

Akizungumzia idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwenye Msikiti huo mkubwa zaidi wa Tehran katika kumbukumbu hizo za jana Alkhamisi, Rais Pezeshkian amesema: "Tunaahidi kwamba tutaendelea na njia ya wapendwa hawa kwa nguvu zetu zote... Tumesimama kupambana na mabeberu na wakandamizaji na hatutolegeza kamba katika njia hiyo."

Amesema: "Jenerali Soleimani alikuwa mfano wa kuigwa usio na kifani katika maadili, uaminifu, ujasiri, kupigania haki na kuwatetea wanaodhulumiwa. Kilichotuleta pamoja leo hapa ni njia ambayo lazima tuipite, na njia hii si nyingine ila ni njia ya mashahidi wa Muqawama."

Kabla ya hapo, kumbukumbu ya mwaka wa 6 tangu kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq ya al Hashd al Sha'abi ilikuwa imefanyika katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Hauli hiyo iliyofanyika kwa hima ya ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Baghdad ilihudhuriwa na shakhsia mbalimbali wa kisiasa, Maulamaa na baadhi ya wawakilishi wa mataifa mbalimbali ikiwemo Russia.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, aliuawa shahidi Januari 3, 2020 katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq ya al Hashd al Sha'abi na wanamapambano wengine wanane, wakati alipoelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.