Vipi IRGC Imefikia Kuwa na Nguvu na Uwezo Unaoshuhudiwa Hivi Sasa?
Maadhimisho ya mwaka huu ya kutimia miaka 48 ya kuasisiwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC yametoa mguso zaidi katika duru za kisiasa na za vyombo vya habari kuliko ilivyowahi kushuhudiwa katika maadhimisho ya miaka iliyopita.
Katika siku arubaini za mapambano ya kihamasa, IRGC, ikiwa bega kwa bega na vikosi vingine vya ulinzi, ilitoa vipigo vikali na vya kushangaza kwa utawala wa Kizayuni na Marekani.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na Jeshi la Iran, ni sehemu ya vikosi rasmi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. IRGC imetajwa kwa uwazi kabisa ndani ya Katiba ya Iran. Jeshi hilo la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lina historia na rekodi ya kipekee inayolipambanua na vikosi vingine vya kijeshi duniani.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilijikuta kwenye kitovu cha misukosuko na dhoruba kali. Hata mwezi mmoja ulikuwa haujapita tangu ushindi wa mapinduzi, wakati makundi mbalimbali ya kisiasa yalipoonyesha muelekeo wa kutaka kuyanyakua mapinduzi hayo. Makundi ya wabeba silaha ya Kimaksi na mrengo wa kushoto, Fadaiyane Khalq, kundi la Munafiqina MKO, na makundi ya wabeba silaha ya kupigania kujitenga katika maeneo ya Kurdistan, Turkmen Sahraa, Khuzestan, na Sistan na Baluchestan, kila moja lilikuwa likitafuta fursa ili liwe kwa namna fulani na sauti na ushawishi katika mustakabali wa Iran.
Jeshi, ambalo lilikuwa limeutumikia utawala wa Pahlavi kwa miaka mingi, lilikuwa halijasambaratika; na Imam Khomeini alitilia mkazo liendelee kudumishwa, lakini ilihitajika kazi kubwa hadi kufikia kwenye hatua ya kuwa jeshi la kimapinduzi. Maadui wa nje nao pia walikuwa wakitafuta fursa ya kuyasambaratisha Mapinduzi kwa njia ya kuchochea mapinduzi ya kijeshi au kuzusha machafuko ya ndani. Ni katika mazingira hayo, ndipo Imam Khomeini, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu mnamo tarehe 22 Aprili, 1979 alitoa amri ya kuundwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC. Kutokana na mtazamo wa kiroho na kidini aliokuwa nao, Imam Khomeini alikuwa tangu mwanzo na dukuduku la mambo mawili: Kwanza ni kudumishwa sura ya wananchi ya Mapinduzi; na pili, ni kuzuia Mapinduzi yasije yakageuzwa kuwa wenzo wa kutumiwa na makundi yanayonyemelea fursa. Kwa hakika, kuundwa kwa IRGC kulitoa jibu kwa madukuduku hayo mawili.
Ripoti za Baraza la Mapinduzi zinaonyesha kuwa kuanzia Machi 1979 hadi Aprili 1979, vilifanyika vikao vizito na vya mtawalia vya wajumbe wa baraza hilo, wafuasi wa Imamu Khomeini, na wanaharakati wa Mapinduzi. Katika vikao hivyo, ulifanyika mjadala wa "kuasisi kikosi chenye mshikamano na cha wananchi"; kikosi ambacho hakitakuwa jeshi, kopi ya kuiga na kujifananisha na makundi ya wapiganaji wa msituni, wala mrengo wa kichama, bali taasisi mpya kabisa iliyojikita katika mihimili mitatu: imani, kuwa ya wananchi, na kuwajibika mbele ya Mapinduzi. Nguzo hizo tatu zinapatikana katika agizo fupi lililotolewa na Imamu Khomeini na katika Hati ya kuasisiwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi.
Amri ya Imamu Khomeini ilisomeka hivi: "Kwa madhumuni ya kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu na matunda yake, litaundwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu." Baada ya miaka 48, ibara hii nyepesi, sasa imebadilika kuwa moja ya nguzo kuu za usalama wa taifa wa Iran. Lakini kuna suali la kujiuliza hapa: Kwa nini IRGC imeundwa ili iwe "Mlinzi wa Mapinduzi" na si "kuilinda nchi" pekee? Jibu linapatikana katika itikadi ya Mapinduzi yenyewe. Mapinduzi ya Kiislamu hayakuwa mapinduzi ya kisiasa tu; yalikuwa mapinduzi ya kijamii, kiutamaduni na ya tunu maalumu pia.
Maadui waliokabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu hawakuwa watumiaji wa vifaru na mizinga tu; vita vyao vikuu vilikuwa vya kulenga utambulisho na tunu na maadili ya Iran. Kwa sababu hiyo, IRGC ilikuwa tangu mwanzo imekabidhiwa misheni, si ya kujizatiti kisilaha tu, lakini pia kulinda imani na utamaduni wa Mapinduzi. Katika miezi ya kwanza ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC ilibeba jukumu la kutekeleza kazi ngumu na ya kuainisha hatima ya nchi: kukabiliana na makundi ya wabeba silaha huko Kurdistan, kuhakikisha usalama unapatikana kusini na mashariki ya nchi, kukabiliana na wabeba silaha wanaopinga mapinduzi katika Jiji la Tehran na miji mikubwa mingine, na kuzima njama za mapinduzi ya kijeshi ikiwemo ya jaribio la Mapinduzi la Nuzhe. Misheni hizo tofauti, tata na ngumu mno hazingeweza kutekelezwa, na njama zake kuzimwa, kwa kutegemea silaha tu na jeshi la klasiki.
Mingi ya migogoro hiyo ilizimwa na kudhibitiwa kwa nguvu laini zisizo za kijeshi na kwa kuyapa sura ya umma mapambano dhidi ya vitisho mbalimbali vilivyoyaandama Mapinduzi ya Kiislamu.
Wakati wa miaka minane ya vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na utawala wa Kibaathi wa Saddam, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi lilibeba jukumu la kuandaa Jeshi la kujitolea la wananchi Basij katika kupambana na jeshi la utawala wa Kibaathi wa Saddam. Vita hivyo vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam hatimaye vilimalizika, na dikteta huyo wa Iraq akalazimika kukubali uhalali wa Mkataba wa Algiers wa 1975. Mkataba wa makubaliano ambao, mnamo Septemba 1980, Saddam alisimama na kuuchana chana mbele ya kamera na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya Iran kwa tamaa ya kuiteka Tehran ndani ya muda wa siku tatu tu.
Miongoni mwa majukumu muhimu zaidi yanayotekelezwa na IRGC, mbali na majukumu ya kulinda mamlaka ya kujitawala ya ardhi na tunu za Mapinduzi ya Kiislamu, ni kuimarisha uwezo wa kijeshi na kiulinzi wa Iran. Kutokana na Iran kubaki peke yake katika uga na medani ya kimataifa, na kwa kuzingatia vikwazo vikali vya silaha ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu, IRGC ilijikita na kuelekeza juhudi zake katika kujiwezesha kumiliki teknolojia ya makombora na ndege zisizo na rubani. Busara na usahihi wa uwekezaji huo umedhihirika katika operesheni nne za Ahadi ya Kweli na mapambano dhidi ya majeshi mawili ya kisasa na yanayomiliki silaha za nyuklia, yaani Marekani na utawala wa Kizayuni. Operesheni nne za Ahadi ya Kweli na mapambano ya kihamasa ya siku arubaini ya kukabiliana na uchokozi wa utawala wa Kizayuni na Marekani yameudhihirishia ulimwengu uwezo mkubwa wa Iran wa kuzuia hujuma na kuwashikisha adabu wachokozi.../