Iran yaikosoa Israel na Marekani kwa kuua watoto vitani
Iran imekosoa vikali Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuwaua watoto wasio na hatia katika nchi mbalimbali kupitia uhalifu wa kivita na uvamizi wa kijeshi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, ametoa kauli hiyo katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X siku ya Alhamisi, kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Walioathiriwa na Uchokozi.
Amesema siku hiyo inahuisha kumbukumbu ya watoto waliopaswa kuwa na ndoto, kusoma na kujenga mustakabali wao, lakini wakawa wahanga wa uhalifu wa kivita, uvamizi na mashambulizi ya mabomu kabla hata hawajapata fursa ya kujua maisha.
Ameongeza kuwa: “Kuanzia Gaza na Ukingo wa Magharibi hadi Beirut, Minab, Lamerd, Tehran na maeneo mengine mengi nchini Iran na duniani, popote pale watoto walikouawa kwa mabomu na makombora ya Marekani na utawala wa Kizayuni, ukweli unabaki ule ule: hakuna lengo la kijeshi, hakuna maslahi ya kisiasa, wala kisingizio chochote cha kiusalama kinachoweza kuhalalisha mauaji ya watoto.”
Kauli hiyo inaashiria mashambulizi mabaya ya Marekani na Israel dhidi ya shule ya msingi katika mji wa Minab na ukumbi wa michezo mjini Lamerd nchini Iran tarehe 28 Februari 2026.
“Watoto si wahusika wa vita wala si zana za vita. Wao ni dhamiri hai ya ubinadamu. Kila mtoto anayepoteza maisha au kujeruhiwa vibaya ni kana kwamba sehemu ya ubinadamu wetu wa pamoja inazikwa,” alisema.
Baghaei pia ameambatanisha ujumbe wake na picha ya Mahya Sedighi Saber, aliyeuawa shahidi katika mji wa Astaneh-ye Ashrafiyeh kaskazini mwa Iran mwaka uliopita wakati wa vita vya kwanza vya uchokozi vya Marekani na Israel.
Marekani na utawala wa Israel zilianzisha shambulio lao la kwanza la kijeshi lisilo halali dhidi ya Iran mwezi Juni 2025, lililodumu kwa siku 12. Uvamizi wao wa pili ulianza mwishoni mwa Februari na kusimamishwa mapema mwezi Aprili kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyopatanishwa na Pakistan.
Katika matukio yote mawili, mapambano imara ya Iran yaliyojumuisha mashambulizi yake ya kulipiza kisasi kwa mafanikio yaliwalazimisha maadui kukubali usitishaji wa mapigano.