Foreign Policy: Chuki dhidi ya Wakristo imeongezeka huko Israel
-
Askari wa Israel akivunja sanamu la Yesu Kristo, kusini mwa Lebanon
Uchunguzi uliofanywa na baadhi ya vyombo vya habari umebaini kuwa chuki na hujuma dhidi ya Wakristo vimeongezeka huko Israel.
Uchunguzi huo unaonyesha kuwa sera hizo za kibaguzi za Wazayuni wa Israel zimevuka mipaka ya kuwashambulia na kuwaua Waislamu wa Palestina na sasa zinawalenga Wakristo na wasio Wayahudi ndani ya Israel kwenyewe.
Mwandishi wa Kitaliano, Giovanni Legorano anasema kwamba shambulio la kikatili dhidi ya mtawa wa Kifaransa huko Quds (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu mwishoni mwa Aprili halikuwa tukio la pekee, bali ni dalili ya ongezeko la kutisha la chuki dhidi ya Wakristo ndani ya Israel, huku kukiwa na ongezeko la siasa kali za kizalendo na kidini na mgawanyiko unaozidi kuwa mbaya katika utawala huo.
Kwa mujibu wa jarida la Marekani la Foreign Policy, tukio hilo limeonyesha ongezeko la unyanyasaji wa maneno na wa kimwili dhidi ya Wakristo na kuvunjia heshima alama na nembo za kidini za Kikristo, vitendo ambavyo wakosoaji wanasema mara nyingi vinapita hivi hivi bila wahusika kuchukuliwa hatua.
Kwa mujibu wa data za Kituo cha Ufuatiliaji wa Uhuru wa Kidini, shirika la Kiyahudi la Israel linalopokea simu ya dharura za malalamiko ya Wakristo, idadi ya matukio ya hujuma na uadui yaliyorekodiwa dhidi ya Wakristo iliongezeka hadi 181 mwaka wa 2025, ikilinganishwa na 107 mwaka wa kabla yake. Matukio haya ni pamoja na kutemewa mate, matusi ya maneno, uharibifu wa milki na mali za Wakristo, mashambulizi ya kimwili, na unyanyasaji mtandaoni.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa, mwanzilishi wa kituo hicho, Yeska Harani, anasema idadi halisi ya ukatili unaofanywa huko Israel dhidi ya Wakristo inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na visa vingi kutoripotiwa.