Ayatullah Khamenei: Kuna ulazima wa kuongeza uwezo wa kushambulia na wa kujilinda
(last modified Wed, 31 Aug 2016 14:50:51 GMT )
Aug 31, 2016 14:50 UTC
  • Ayatullah Khamenei: Kuna ulazima wa kuongeza uwezo wa kushambulia na wa kujilinda

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa Iran kuongeza uwezo wa kushambulia sambamba na uwezo wa kujihami na kujilinda.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran amesema hayo leo alipotembelea maonyesho ya vifaa vilivyotengenezwa na Wizara ya Ulinzi ya Iran na kusisitiza kwamba, kuongeza uwezo wa kujilinda na kushambulia ni haki ya wazi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, ustawi na maendeleo ya teknolojia ya kujilinda ya Iran ni natija ya harakati kubwa ya kielimu ya taifa hili katika kipindi cha miaka 12 iliyopita.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, wasomi vijana wa Iran wamefanikiwa kuvuka mistari myekundu ya elimu na kuna ulazima wa kuendelezwa harakati hii kwa nguvu kubwa kwani maendeleo katika uga wowote utakuwa ni ufunguo wa maendeleo mapya katika nyanja nyingine.

Ayatullah Khamenei. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kusisitiza juu ya udharura wa kuongezwa uwezo wa kiulinzi amesema kuwa, katika ulimwengu ambao madola yanayotumia mabavu, ubeberu na ubinaadamu pamoja na maadili vinashuhudiwa kwa uchache mno, madola ambayo hayasiti kuvamia mataifa mengine, kuwauwa watoto wasio na hatia, kupanua sekta ya kujilinda na kuwa na uwezo zaidi wa kushambulia ni jambo la kawaida. 

Ayatullah Khamenei ameashiria kukasirika baadhi ya madola makubwa kutokana na Iran kununua vifaa vya kiulinzi kutoka kwa baadhi ya nchi na kusema kwamba, madola hayo yanadai kuwa na insafu na kutumia akili na yanazungumzia ustahiki wa kimaadili wa mataifa mengine ya kuwa au kutokuwa na baadhi ya vifaa vya kiulinzi katika hali ambayo, yenyewe hayafungamani na msingi wowote ule wa kimaadili.