Iran yatangaza tarehe ya uchaguzi wa Rais
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uchaguzi ujao wa Rais nchini utafanyika tarehe 18 Mei mwakani.
Abdolreza Rahmani Fazli, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran alisema hayo jioni ya jana Jumatano na kuongeza kuwa, tarehe 18 Mei mwaka 2017 ndiyo itakayokuwa siku ya uchaguzi wa 12 wa Rais nchini Iran.
Ameongeza kuwa, mipango na ratiba maalumu zimeandaliwa kwa kushirikiana na Baraza la Kulinda Katiba la Iran kwa ajili ya kuendesha uchaguzi huo kwa njia bora kabisa.
Abdolreza Rahmani Fazli ameongeza kuwa, baada ya kufanyika mazungumzo baina ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Baraza la Kulinda Katiba imeamuliwa kuwa tarehe 29 Ordibesht 1396 (Mei 18, 2017) iwe siku ya kufanyika uchaguzi wa Rais, mabaraza ya Kiislamu na chaguzi ndogo za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran.
Kwa mujibu wa sheria, uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hufanyika mara moja kila baada ya miaka minne na yeyote anayechaguliwa vipindi viwili mfululizo, huwa hana haki ya kisheria kugombea kipindi kinachofuata cha uchaguzi.