Zarif akosoa masharti ya Ujerumani kwa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i16504-zarif_akosoa_masharti_ya_ujerumani_kwa_iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amekosoa vikali matamshi ya hivi karibuni ya Waziri wa Uchumi wa Ujerumani aliyesema kuwa Berlin inaweza kuimarisha uhusiano wake na Tehran kwa sharti kuwa Jamhuri ya Kiislamu iutambue utawala haramu wa Israel.
(last modified 2026-05-13T18:57:29+00:00 )
Oct 02, 2016 04:43 UTC
  • Zarif akosoa masharti ya Ujerumani kwa Iran

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amekosoa vikali matamshi ya hivi karibuni ya Waziri wa Uchumi wa Ujerumani aliyesema kuwa Berlin inaweza kuimarisha uhusiano wake na Tehran kwa sharti kuwa Jamhuri ya Kiislamu iutambue utawala haramu wa Israel.

Muhammad Javad Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu ni taifa huru ambalo haliwezi kushurutishwa jambo lolote na nchi za kigeni na kusisitiza kuwa sera za nchi hii ziko wazi.

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran

Dakta Zarif amesema licha ya kwamba Iran ya Kiislamu ni taifa linalopenda amani, lakini daima imekuwa ikipinga ubeberu na mashinikizo ya nchi ajinabi katika muda wa miaka 37 iliyopita.

Katika mahojiano na jarida la kila wiki la Der Spiegel Ijumaa iliyopita,Sigmar Gabriel, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani alisema uhusiano wa Iran na Ujerumani unaweza kuimarika iwapo Tehran itatambua na kuheshimu uwepo wa Israel.

Bendera za Iran na Ujerumani

Kadhalika hapo jana katika radiamali yake kwa matamshi ya Waziri wa Uchumi wa Ujerumani aliyesema kuwa uhusiano kati ya Berlin na Tehran unaweza kurejea katika hali ya kawaida na hata kuimarika zaidi iwapo Jamhuri ya Kiislamu itautambua utawala wa Kizayuni wa Israel, Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema katu nchi hii haitoacha kuiunga mkono Palestina. Alisisitiza kuwa, uhusiano kati ya nchi mbili hizi umejengeka katika misingi ya heshima na maslahi ya pande mbili.