Iran: Hatutaki ushauri wa kigeni juu ya uchaguzi wetu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i1768-iran_hatutaki_ushauri_wa_kigeni_juu_ya_uchaguzi_wetu
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ni nchi huru isiyohitaji ushauri wa nchi za kigeni juu ya uchaguzi wa Bunge na Baraza la Wataalamu uliopangwa kufanyika siku ya Ijumaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 23, 2016 04:20 UTC
  • Iran: Hatutaki ushauri wa kigeni juu ya uchaguzi wetu

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ni nchi huru isiyohitaji ushauri wa nchi za kigeni juu ya uchaguzi wa Bunge na Baraza la Wataalamu uliopangwa kufanyika siku ya Ijumaa.

Hossein Jaberi Ansari amesema kwamba taifa la Iran limejiandaa kupanua izza na utukufu wa Jamhuri ya Kiislamu katika uga wa kieneo na kimataifa; kutokana na namna wananchi watakavyojitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi wao wawapendao. Akijibu ushauri uliotolewa hivi karibuni na Shirika la Habari la Uingereza BBC wa kuwataka wananchi wa Iran wawachague wagombea fulani katika uchaguzi wa Baraza la Wataalamu, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Msimamo wetu uko wazo, kwamba moja ya mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ni uhuru wa kujitawala na uhuru wa maoni na kwa msingi huo, taifa la Iran halina haja na ushauri kutoka asasi za kigeni kuhusu zoezi hilo la kidemokrasia."

Wairani milioni 54, wametimiza masharti ya kupiga kura katika uchaguzi ujao wa mwezi huu wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran na Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema mipango imekamilika kwa ajili ya uchaguzi huo. Ali Ridha Rahman Fadhli amesema, masanduku 129,000 ya kupigia kura yamewekwa katika vituo 53,000 vya kupigia kura kote Iran. Aidha amesema zaidi ya maafisa nusu milioni watasimamia zoezi la uchaguzi mwaka huu.