Iran: Tutajibu hatua yoyote ya Marekani ya kuvunja JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i20500-iran_tutajibu_hatua_yoyote_ya_marekani_ya_kuvunja_jcpoa
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, kama Marekani itarefusha vikwazo dhidi ya Iran, basi Jamhuri ya Kiislamu itaongeza kiwango cha urutubishaji wake wa urani kwa "SWU" laki moja na 90 elfu.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 30, 2016 12:59 UTC
  • Alauddin Burujerdi, Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje wa Bunge la Iran.
    Alauddin Burujerdi, Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje wa Bunge la Iran.

Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, kama Marekani itarefusha vikwazo dhidi ya Iran, basi Jamhuri ya Kiislamu itaongeza kiwango cha urutubishaji wake wa urani kwa "SWU" laki moja na 90 elfu.

Alauddin Burujerdi amesema hayo wakati alipohojiwa na mwandishi wa Radio Tehran na kuongeza kuwa, kurefushwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni uvunjaji wa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la JCPOA. Vile vile amesema, Bunge la Iran linajadili suala la Marekani la kutoheshimu ahadi zake na namna ya Tehran inavyoweza kukabiliana na kitendo hicho cha Marekani cha kukosa uaminifu. Amesema, Bunge la Iran litapasisha sheria ya kuiruhusu Tehran ijibu hatua yoyote itakayochukuliwa na Marekani ya kuvunja makubliano ya JCPOA.

Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje wa Bunge la Iran ameongeza kuwa, suala la nyuklia ni kadhia ya taifa zima la Iran na inazijumuisha pande zote ikiwemo Serikali, Bunge na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu na wote wako kitu kimoja katika suala hilo.

Majlis ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran)

 

Vile vile amesema, Marekani ni moja tu ya nchi sita zilizotia saini makubaliano hayo ya nyuklia baina yao na Iran na kwa mujibu wa taarifa alizo nazo, nchi za Ulaya zilizotia saini makubaliano hayo haziko tayari kuona JCPOA inafutwa na ni wazi pia kuwa, Russia na China nazo haziwezi kukubaliano na hatua kama hizo za Marekani.

Burujerdi amesisitiza kuwa, hatua yoyote mbaya itakayochukuliwa na Marekani itakuwa ni kwa madhara ya nchi hiyo na hakuna mtu yeyote atakayeweza kuilaumu Iran iwapo itachukua hatua kukabiliana na uvunjaji wa makubaliano ya JCPOA unaofanywa na Marekani.