Mkuu wa tume ya uchaguzi Iran: Hakuna matokeo yoyote yaliyofutwa
Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Iran amesema kuwa, hadi hivi sasa hakuna matokeo yoyote ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu yaliyofutwa.
Mwandishi wa Radio Tehran amemnukuu Bw. Mohammad Hossein Moghimi akisema hayo leo jioni mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa, zoezi la kuhesabu kura lingali linaendelea.
Amesema kuwa, matokeo ya kuhesabu kura wataendelea kutangaziwa wananchi na Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB.
Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Iran ameongeza kuwa, hadi hivi sasa haijajulikana zoezi la kuhesabu kura litamalizika wakati gani.
Uchaguzi wa Bunge la Kumi la Iran na Baraza la Tano la Wanavyuoni Wataalamu linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu lilifanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 26 Februari.