Boroujerdi: Siasa za Marekani dhidi ya Iran zingali za kihasama
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) amesema Marekani imekuwa ikiendeleza jinai zake dhidi ya taifa la Iran tangu huko nyuma hadi hivi sasa na kusisitiza kwamba sera za nchi hiyo kuhusiana na taifa la Iran zingali za kiadui na kihasama.
Alaeddin Boroujerdi ameashiria kuwepo kwa washauri 60,000 wa Kimarekani hapa nchini katika zama za kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu waliokuwa wakisimamia masuala ya utawala na kufafanua kuwa mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 18 Agosti 1953 pamoja na makumi ya jinai zingine zimewafanya kila mara wananchi wa Iran wabainikiwe kwa uwazi kuhusu dhulma na udikteta wa Marekani.
Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Sera za Nje ya Bunge ameongeza kuwa leo hii kwa rehma za Mwenyezi Mungu milingano yote imebadilika; na Marekani, ambayo inaonekana kuwa ndilo dola kuu katika mlingano wa kimataifa inadhalilishwa na kufedheheshwa na ushujaa wa vijana wa Iran katika Ghuba ya Uajemi.
Aidha ameashiria njama na mashinikizo ya kiuchumi ya maadui dhidi ya Iran na kusisitiza kwamba: Bila ya shaka yoyote taifa ambalo limeweza kuyashinda madola yote yenye nguvu katika vita vya kijeshi, litamshinda adui katika vita vya kiuchumi pia.
Boroujerdi ameeleza pia jinsi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivyo na usalama thabiti na kufafanua kwamba katika hali ambayo Mashariki na Magharibi pamoja na nchi nyingi za eneo hazina amani na usalama, Iran ya Kiislamu ina amani na usalama kamili kiasi cha kuwastaajabisha hata wavurugaji amani na waungaji mkono wa magaidi, yaani Marekani na Ulaya…/