Iran yalaani miripuko ya mabomu ya nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i21166-iran_yalaani_miripuko_ya_mabomu_ya_nchini_nigeria
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani miripuko ya mabomu iliyotokea nchini Nigeria na kupelekea watu wengi kuuawa bila ya hatia.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Dec 10, 2016 23:37 UTC
  • Iran yalaani miripuko ya mabomu ya nchini Nigeria

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani miripuko ya mabomu iliyotokea nchini Nigeria na kupelekea watu wengi kuuawa bila ya hatia.

Bahram Qassemi ameongeza kuwa, daima Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vitendo vya aina yoyote ile vya kigaidi popote pale ulimwenguni na siku zote inahimiza kuweko ushirikiano wa kweli wa kupambana na magenge ya kigaidi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha ametoa mkono wa pole kwa serikali na taifa la Nigeria kutokana na miripuko hiyo na kusema kuwa, wananchi wa Iran wako pamoja na familia za wahanga wa miripuko hiyo huko Nigeria katika huzuni.

Miripuko ya mabomu imesababisha hasara kubwa za roho na mali nchini Nigeria

 

Miripuko ya mabomu iliyotokea siku ya Ijumaa katika soko moja la mji wa Madagali, kwenye jimbo la Adamawa, kaskazini mashariki mwa Nigeria imepelekea watu 56 kuuawa na zaidi ya 170 wengine kujeruhiwa.

Msemaji wa jeshi la Nigeria, Badare Akintoye amesema kuwa, wanawake wawili waliokuwa wamevaa mabomu ndio waliojiripua kwenye soko hilo na kusababisha maafa hayo makubwa.

Siku chache zilizopita jumuiya mbalimbali likiwemo shirika la Amnesty International zilitangaza kuwa, wanawake na wasichana wa Nigeria waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram wanatumiwa katika mashambulizi ya kigaidi ya kujiripua kwa mabomu hasa kwenye mikusanyiko ya watu wengi.

Hadi hivi sasa mamia ya maelfu ya raia wa Nigeria wamekimbilia nchi za Cameroon, Chad na Niger, kutokana na kushadidi mashambulio ya Boko Haram katika majimbo ya Adamawa, Yobe na Borno ya nchini Nigeria.