Jeshi la Iran lazindua drone za kivita, upelelezi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i21355-jeshi_la_iran_lazindua_drone_za_kivita_upelelezi
Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limezindua ndege zisizo na rubani (drone) mbili zilizotengenezwa hapa nchini zenye uwezo wa kivita na upelelezi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 13, 2016 12:46 UTC
  • Jeshi la Iran lazindua drone za kivita, upelelezi

Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limezindua ndege zisizo na rubani (drone) mbili zilizotengenezwa hapa nchini zenye uwezo wa kivita na upelelezi.

Droni hizo zimezinduliwa katika siku ya mwisho ya mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la Muhammad Rasulullah IV kusini mashariki mwa Iran.

Moja ya droni hizo imepewa jina la Oghab na ina uwezo wa kivita ikiwa ni pamoja na kusheheni makombora ya angani kwa nchi kavu.

Droni ya pili inajulikana kama Shahin na ina uwezo wa kufanya upelelezi na kukusanya taarifa za siri za harakati za adui. Droni hiyo inaweza kubakia angani kwa muda wa masaa 24 mfululizo.

Msemaji wa mazoezi hayo Jenerali Seyyed Kamal Peyambari amesema droni hizo zimefanyiwa majaribio yaliyofana katika mazoezi hayo ambayo pia yalitumiwa kufanyia majaribio silaha mbali mbali.

Mazoezi ya kijeshi kusini mashariki mwa Iran

Katika miaka ya hivi karibuni Iran imepata mafanikio makubwa katika sekta ya ulinzi huku ikijitosheleza kwa kiasi kikubwa katika zana za kujihami. Aidha Jeshi la Iran hufanya mazoezi ya mara kwa mara kwa ajili ya kubaini uwezo wa vikosi vyake na pia kufanyia majaribio zana mpya za kivita. Jamhuri ya Kiislamu inasisitiza kuwa uwezo wake wa kijeshi si tishio kwa nchi zingine bali sera yake ya ulinzi imejengeka katika msingi wa kujihami.