Velayati: Iran ni kimbilio salama la Waislamu wote
Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislami ni kimbilio na nchi salama zaidi kwa Waislamu wote.
Dakta Ali Akbar Velayati aliyasema hayo jana usiku katika Kongamano la Kimataifa la Utamaduni na kubainisha kuwa, uwepo wa makundi ya kigaidi na kitakfiri kama vile Daesh/ISIS, al-Nusra na al-Qaeda katika nchi za Kiislamu ni ithibati kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo kimbilio pekee la Waislamu duniani.
Amesema lengo la makundi hayo yenye misimamo ya kufurutu ada ni kupaka matope taswira halisi ya Uislamu, na ndiposa yamekuwa yakifanya jinai za kutisha na zilizo dhidi ya ubinadamu wakitumia jina la dini hiyo tukufu.
Dakta Velayati ambaye pia ni Mshauri Mkuu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei ameashiria namna Hillary Clinton, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alivyokiri wakati wa kuanza muhula wa kwanza wa Rais Barack Obama wa nchi hiyo kuwa: Wao ndio waliounda Daesh kwa lengo la kuvuruga usalama katika uliwengu wa Kiislamu.
Huku akivitaja vyombo vya habari vya Magharibi kama "Pembe ya Shetani" ameongeza kuwa, Uislamu tu ndio dini inayopambana na ukafiri na unafiki na kwamba asasi na mashirika ya dini za Kimagharibi kama vile Vatican yameshindwa kukabiliana kwa dhati na jinamizi hilo. Amesema ni kwa msingi huo ndiposa vyombo vya habari vya Magharibi vimekuwa vikiyataja makundi hayo ya kigaidi kama magenge ya Kiislamu yenye misimamo mikali ili kuchafua utambulisho halisi wa dini hii. Amesisitiza kuwa, Uislamu ni dini ya amani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kimbilio salama la Waislamu wote.
Hapo jana shirika la habari la Ufaransa AFP lilitangaza kuwa, wafuasi wa dini za wachache wakiwemo Wakristo wanaishi kwa usalama mkubwa nchini Iran na kwamba nchi hiyo ni katika nchi zenye usalama mkubwa zaidi kwa watu wa dini za wachache kwenye eneo la Mashariki ya Kati.