Rais Rouhani: Iran inakaribisha kwa mikono miwili usitishaji vita nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i22519-rais_rouhani_iran_inakaribisha_kwa_mikono_miwili_usitishaji_vita_nchini_syria
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inakaribisha kwa mikono miwili usitishaji vita nchini Syria na kusisitiza kwamba, kuna haja ya kuwa macho ili usitishaji vita huo usitumiwe kama fursa ya kujiimarisha makundi ya kigaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 31, 2016 13:54 UTC
  • Rais Rouhani: Iran inakaribisha kwa mikono miwili usitishaji vita nchini Syria

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inakaribisha kwa mikono miwili usitishaji vita nchini Syria na kusisitiza kwamba, kuna haja ya kuwa macho ili usitishaji vita huo usitumiwe kama fursa ya kujiimarisha makundi ya kigaidi.

Raias Hassan Rouhani amesema hayo alasiri ya leo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Walid al-Muallim, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria na ambapo sambamba na kutoa mkono wa kheri na pongezi kwa serikali, jeshi na wananchi wanamuqawama wa Syria katika mapambano dhidi ya ugaidi hususan katika mji wa Halab amesema kuwa, ushindi wa Halab ni ujumbe kwa magaidi kwamba, katu magaidi hao hawawezi kufanikiwa kutokana na kuchagua kwao njia isiyo sahihi ya kutenda jinai na kumwaga damu.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Syria

Rais wa Iran amesema kuwa, baada ya ushindi na ukombozi wa mji wa Halab, kumejitokeza mazingira mazuri ya kuchukuliwa hatua dhidi ya magaidi na kufanyika harakati za kisiasa kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu nchini Syria. Rais Rouhani amesema kuwa, ana matumaini hatua zitakazochukuliwa kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria na mazungumzo ya amani zitaheshimu mamlaka ya Syria, kurejeshwa amani na kulindwa ardhi yote ya nchi hiyo.

Kwa upande wake, Walid al-Muallim, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria amempatia Rais Rouhani salamu na ujumbe wa shukrani wa Rais Bashar al-Assad kwa serikali na taifa la Iran na kusema kuwa, hakuna shaka yoyote kwamba, misaada na himaya ya pande zote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa na itaendelea kuwa na taathira muhimu mno katika kuimarisha moyo wa muqawama na mapambano wa taifa la Syria mbele ya magaidi.