Vyuo vikuu vitatu vya Iran vyaingia katika vyuo bora 500 duniani
Chuo Kikuu cha Zanjan, Ferdous cha Mash'had na chuo kikuu cha Tehran vimeingia katika orodha ya taasisi ya mfumo bora wa kielimu duniani ya 'Green Metric'
Taarifa iliyotolewa na taasisi hiyo juu ya ripoti ya mwaka jana 2016 kuhusiana na taarifa ya ustawi wa taasisi za utafiti wa kielimu duniani imeviorodhesha vyuo vikuu hivyo vitatu vya nchini hapa kuwa vilivyoweza kufikia kiwango stahiki cha elimu inayotakiwa na taasisi ya Green Metric.
Taasisi hiyo hutumia viashiria sita muhimu vikiwemo vya 'Mazingira na Miundombinu', 'Nishati na Mabadiliko ya Tabia Nchi', 'Usimamizi wa Taka', 'Maji' 'Usafirishaji' na 'Elimu' kama kipimo kwa ajili ya kufahamu ustawi wa taasisi husika. Aidha Green Metric inakusudia kuionyesha dunia mazingira na siasa zinazohusiana na mazingira ya hali ya hewa na maendeleo endelevu katika vyuo vikuu vya sasa kote ulimwenguni.
Kwa mwaka, zaidi ya taasisi elfu 10 hufanyiwa uchunguzi duniani na kuorodheshwa baadaye na taasisi hiyo sambamba na kutangazwa katika mtandao wake. Kwa mujibu wa Green Metric, Chuo Kikuu cha Zanjan, kimeshika nafasi ya 75 kwa kupata kura 5971, Chuo Kikuu cha Ferdous cha Mash'had kimeshika nafasi 238 kwa kupata kura 4484 huku kile cha Tehran kikishika nafasi ya 431 kwa kupata kura 3209.