Jeshi la majini la Iran lawatimua maharamia wa Somalia
Maharamu kutoka Somalia waliojaribu kuteka nyara meli ya mizigo ya Iran wametimuliwa na manwoari za Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne, jeshi la Wanamaji la Iran limesema limetimua boti 11 za maharamia Wasomali katika Lango Bahari la Babul Mandab ambao walikuwa wamelenga kuihujumu na kuiteka nyara meli ya mizigo ya Iran. Manowari za Iran za Msafara wa 44 zilifika katika eneo la hujuma hiyo na kuwatimua maharamia hao.
Msafara huo wa 44 wa Manowari Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliekelea katika maji ya kimataifa Oktoba 5 kulinda njia za baharini zinazotumiwa na meli za kibiashara.
Hadi sasa msafara huo ambao unajumuisha manowari za Alvand na Bushehr umenusuru meli kadhaa za Iran na za kigeni ambazo zilishambuliwa na maharamia wa Kisomali wakitaka kuziteka nyara.
Akizungumza jana, Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran alisema kuwa suala linalopewa umuhimu zaidi na jeshi hilo kwa sasa ni kulinda usalama wa Ghuba ya Aden, Bahari Nyekundu na lango bahari la Bab El Mandab.
Admeli Habibollah Sayyari alisema kuwa Jeshi la Majini la Iran hadi sasa limesindikiza na kudhamini usalama wa meli 3m800 za kibiashara na zinazobeba mafuta za Iran na nyingine elfu 25 za kigeni katika lango bahari la Bab El Mandab na Ghuba ya Aden.