Russia: Hakuna chochote kinachoweza kuvuruga uhusiano wa Tehran na Moscow
Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema uhusiano wa pande mbili wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hauwezi kuyumbishwa wala kuathiriwa na 'nguvu za nje' au upande wa tatu.
Ryabkov amesema uhusiano wa Moscow na Tehran uko imara na kwamba nchi mbili hizi mbali na ujirani, zimekuwa zikishirikiana kwa karibu katika mambo mbali mbali kama vita dhidi ya ugaidi.
Mwanadiplomasia huyo wa Russia amesema ni kutokana na muamala mzuri na uhusiano wa karibu usio na mithili kati ya nchi yake na Iran ulifanya Moscow tangu awali iunge mkono makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayofahamika kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Amesema Russia ina uhusiano mzuri wa uitifaki na Iran, na kwamba nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Iran katika mambo kadhaa wa kadha kama vile kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika uga wa biashara na uchumi sambamba na kutekeleza mapatano ya Vienna ya JCPOA.
Hivi karibuni, Russia ilisema haikubaliani na mtazamo wa serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani wa kuitambulisha Iran kama "dola la kigaidi". Katika mahojiano na televisheni ya Fox News siku chache zilizopita, Trump alidai kuwa Iran ni "dola nambari moja la kigaidi".
Akijibu matamshi hayo, msemaji wa Ikulu ya Russia, Kremlin, Dmitry Peskov alisema: "Moscow hatukubaliani na dhana hii ya watawala wa Washington".