Wanaharakti wanaounga mkono Palestina duniani wakutana Tehran
Kongamano la kimataifa la Mashirika ya Kiraia na wanaharakati wanaounga mkono mapambano ya ukombozi wa Palestina limeanza leo Tehran ,mji mkuu wa Iran.
Mkutano huo wa siku moja unawashirikisha wawakilishi wa zaidi ya mashirika 30 ya kiraia yanayounga mkono Palestina kutoka maeneo yote ya dunia na mada kuu ya mkutano huo ni kujadili njia ambazo mashirika ya kiraia yanaweza kuzitumia kuunga mkono Intifadha au mwamko wa watu wa Palestina.
Mkuntano huo utajadili njia za kuwepo mpango wa kivitendo wa pamoja na umuhimu wa harakati katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuunga mkono Palestina kati ya mambo mengine.
Mkutano huo wa wanaharakati wanaounga mkono Palestina unafanyika siku moja baada ya kumalizika mkutano wa sita wa kimataifa wa kuunga mkono Intifadha ya Palestina uliofanyika hapa Tehran na kuwaleta pamoja washiriki zaidi ya 700 kutoka nchi 80 duniani.
Mkutano huo ulimalizika kwa tamko la mwisho ambalo linasisitizia udharura wa kulindwa kadhia ya Palestina ambayo ni kipaumbele cha kwanza cha nchi za ulimwengu wa Kiislamu na za Kiarabu na ndilo zingatio kuu la fikra za walio wengi duniani. Aidha washiriki waliunga mkono kuunda nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Quds Tukufu.