Ayatullah Kermani: Kadhia ya Palestina; kipaumbele cha Iran na Ulimwengu wa Kiislamu
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo katika mji wa Tehran amesema kuwa kadhia ya Palestina inapewa uzito katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ni kipaumbele cha Ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Muhammad Ali Muvahedi Kermani ameashiria katika hotuba za Sala ya Ijumaa hii leo hapa Tehran kufanyika Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Kuiunga Mkono Intifadha ya Palestina hapa Tehran na kuongeza kuwa, kama inavyosisitizwa katika dini ya Uislamu kuwa ni haramu Waislamu na ardhi za Kiislamu kudhibitiwa na makafiri, suala la kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kupambana na kughusubiwa ardhi zao na utawala wa Kizayuni ni katika kipaumbe cha siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Muvahedi Kermani amebainisha namna maslahi ya taifa la Iran yanavyofungamana na suala la Palestina na kueleza kuwa, jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina, mauaji, kuwafanya raia hao kuwa wakimbizi na kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao, ni mambo ambayo kamwe hayawezi kusahaulika. Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo katika mji wa Tehran ameashiria mpango wa kuasisi utawala haramu wa Israel katika ardhi za Palestina na kueleza kuwa, Uingereza ndiyo iliyobuni mpango wa kuasisiwa dola la Kiyahudi- Kizayuni katika ardhi za Wapalestina kwa lengo la kuipa utambulisho jamii iliyo kinyume cha sheria na kisha Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zikaunga mkono mpango huo.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ameendelea kusema kuwa, hatua ya kuidhihirisha Iran kuwa ni tishio, kuwepo chuki dhidi ya Uislamu na kumvunjiwa heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu Muhammad (S.A.W) huko Ulaya, ni natija ya kuwa na ushawishi lobi za Wazayuni katika ulimwengu wa Ulaya na Marekani.