Ayatullah Javadi Amoli: Marekani itasambaratika kama ulivyosambaratika Umoja wa Kisovieti
Ayatullah Abdullah Javadi Amoli, mwanazuoni mkubwa na Marjaa Taqlidi wa mjini Qum Iran amesema kuwa, Marekani itasambaratika kama ulivyosambaratika Umoja wa Kisovieti.
Ayatullah Javadi Amoli amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo mjini Qum na baadhi ya shakhsia wa kiutamaduni wa Russia na kusisitiza kwamba, hatima ya Marekani itakuwa kama hatima ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti.
Akijibu swali kuhusiana na barua ya kihistoria ya Imam Khomeini MA kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa wakati huo huo wa Umoja wa Kisovieti, Ayatullah Javadi Amoli amesema kuwa, wakati sauti ya Uislamu iliposikika kutoka Iran, ulikuwa mwito wa ndani ya moyo ambao ulikuwa ukitambuliwa na wakati wito huu unapozingatiwa, basi utawavutia wote.
Januari mwaka 1989, barua ya kihistioria ya Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwasilishwa kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti akimlingania dini ya Kiislamu na kumtaka aachane na fikra za Kimaksi na kwamba, Uislamu na kumuabudu Mungu Mmoja ndio njia pekee ya kumuokoa mwanadamu.
Sehemu moja ya barua hiyo iliyowasilishwa na Ayatullah Javadi Amoli ilisema: Tatizo kuu la nchi yako si suala la umiliki, uchumi wala uhuru, bali ni kutokuwa na imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu; na tatizo hilo ndilo lililoitumbukiza au litakaloitumbukiza Magharibi katika mporomoko wa kimaadili na kuifanya igonge ukuta. Tatizo lenu kubwa ni kupigana vita visivyokuwa na faida dhidi ya Mwenyezi Mungu."
Miaka kadhaa baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti, Gorbachev alionyesha kusikitishwa na kutozingatia tahadhari zilizotolewa na Imam Khomerini MA.