Feb 27, 2017 07:46 UTC
  • Mkutano wa kimataifa wa kupambana na madawa ya kulevya waanza mjini Tehran

Mkutano wa kimataifa wa kupambana na madawa ya kulevya umeanza kufanyika hapa mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na shakhsia mbalimbali wa ndani na wa kimataifa.

Moja ya malengo ya mkutano huo ni kuchunguza mwenendo wa magendo ya madawa ya kulevya kupitia njia ya Balkan na kutafuta njia za kuwa na ushirikiano kwa ajili ya kukabiliana na magendo ya madawa ya kulenya pamoja na uhalifu wa kimataifa.

Jumla ya wawakilishi kutoka nchi 35 za bara la Asia na Ulaya pamoja na wawakilishi 19 kutoka taasisi 19 za kieneo na kimataifa wanashiriki katika mkutano huo.

Maafisa wa Iran baada ya kukamatwa gari lililobeba madawa ya kulevya

Abdolreza Rahmani Fazli, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran na Yury Fedotov Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Kupambana na Madawa ya Kulevya ya Umoja wa Mataifa wanaongoza kikao cha mkutano huo wa kimataifa wa kupambana na magendo ya madawa ya kulevya unaofanyika hapa mjini Tehran.

Mkutano huo unafanyika katika hali ambayo, asasi zinazofungamana na Umoja wa Mataifa zimekiri wazi juu ya hatua kubwa iliyopigwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita dhidi ya magendo ya madawa ya kulevya.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya magendo ya madawa ya kulevya ulimwenguni imetoa mashahidi zaidi ya 3500 waliouawa katika njia ya kupambana na magendo ya madawa ya kulevya. 

Tags