Rouhani: Uhusiano wa Iran na Azerbaijan unastawi na ni wa kistratijia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i25978-rouhani_uhusiano_wa_iran_na_azerbaijan_unastawi_na_ni_wa_kistratijia
Rais Hassan Rouhani amesema uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Azerbaijan ni wa kiudugu na wa kistratijia na kuongeza kuwa kupiga hatua uhusiano wa baina ya pande mbili za Tehran na Baku kwa upande wa mawasiliano wa kisiasa, wa masuala ya kieneo, kimataifa na kiutamaduni ni wenye umuhimu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 05, 2017 13:04 UTC
  • Rouhani: Uhusiano wa Iran na Azerbaijan unastawi na ni wa kistratijia

Rais Hassan Rouhani amesema uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Azerbaijan ni wa kiudugu na wa kistratijia na kuongeza kuwa kupiga hatua uhusiano wa baina ya pande mbili za Tehran na Baku kwa upande wa mawasiliano wa kisiasa, wa masuala ya kieneo, kimataifa na kiutamaduni ni wenye umuhimu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo mbele ya waandishi wa habari hapa mjini Tehran baada ya kikao baina ya jumbe za ngazi za juu za Iran na Azerbaijan alichokiongoza yeye na mgeni wake Rais Ilham Aliev wa Azerbaijan na kubainisha kuwa kuongezeka kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Azerbaijan katika miezi michache iliyopita ni kiashiria cha kustawi uhusiano wa nchi mbili.

Rais Rouhani na mgeni wake katika mkutano na waandishi wa habari

Dakta Rouhani amefafanua kwamba nchi hizi mbili zina nafasi muhimu katika usafirishaji bidhaa baina ya kaskazini na kusini na kwamba hatua ya kwanza muhimu imepigwa katika suala hilo kutokana na kuunganishwa njia ya reli ya Astara – Astara.

Kwa upande wa masuala ya kieneo pia Rais Rouhani amesema Tehran na Baku zina mtazamo mmoja kuhusu masuala ya kieneo na ugaidi na zinaamini kuwa fikra za Uwahabi na Usalafi ni hatari kubwa katika eneo na kwamba inapasa fikra hizo za kigaidi zitokomezwe moja kwa moja.

Kikao cha pamoja cha jumbe za nchi mbili

Kwa upande wake, Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan amewaeleza waandishi wa habari kuwa uhusiano wa karibu wa nchi yake na Iran ni hidaya kwa eneo na kusisitiza kuwa mikutano kadhaa aliyofanya na rais wa Iran katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita inaonyesha jinsi uhusiano wa nchi hizi mbili unavyostawi.

Aidha ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi inazofanya kwa ajili ya kutatua mzozo wa eneo la Karabakh linalogombaniwa na nchi yake na Armenia na kuongeza kuwa kadhia ya Karabakh imefungamana na suala la ardhi yote, uadilifu na insafu ambayo ni masuala yanayotetewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran…/