Rais Rouhani: Vita vya sasa katika nyuga mbalimbali ni Vita vya Irada
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i26108-rais_rouhani_vita_vya_sasa_katika_nyuga_mbalimbali_ni_vita_vya_irada
Rais Hassan Rouhani amesema hakuna silaha yoyote iliyo kubwa zaidi kuliko silaha ya imani, muqawama na umoja wa wananchi na akabainisha kwamba vita vya sasa katika nyuga mbalimbali ni vita vya irada.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Mar 08, 2017 12:54 UTC
  • Rais Rouhani: Vita vya sasa katika nyuga mbalimbali ni Vita vya Irada

Rais Hassan Rouhani amesema hakuna silaha yoyote iliyo kubwa zaidi kuliko silaha ya imani, muqawama na umoja wa wananchi na akabainisha kwamba vita vya sasa katika nyuga mbalimbali ni vita vya irada.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo alipohutubia kongamano la kimataifa la kuwaenzi mashahidi wa Ulimwengu wa Kiislamu na Siku ya Shahidi lililofanyika katika mji wa Mash-had kaskazini mwa nchi.

Amesema, katika kipindi cha miaka minane ya vita vya Kujihami Kutakatifu, vijana wa Kiirani walipata ushindi kwa irada, kama ambavyo Hizbullah ya Lebanon pia ilipata ushindi dhidi ya utawala wa Kizayuni katika vita vya irada.

Rais Rouhani amefafanua kuwa, pasina kuwa na zana za kijeshi, vijana waumini wa Hizbullah waliweza kusimama kidete kukabiliana na utawala dhalimu, ghasibu, muuaji wa watoto na wa kinyama wa Kizayuni katika Vita vya Siku 33 na kuiporomosha haiba ya kimaonesho ya utawala huo.

Baadhi ya washiriki wa kongamano

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria ununuzi wa silaha wa baadhi ya nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi na kubainisha kwamba, ununuzi wa silaha na zana za kisasa za kivita sio unaowezesha kupata ushindi, kwa sababu wananchi wanyonge wa Yemen wameweza kupata ushindi dhidi ya wavamizi kutokana na imani na irada imara na thabiti waliyonayo.

Dakta Rouhani amesisitiza pia kwamba si silaha pekee zinazoipa ushindi Iran mbele ya Marekani, utawala wa Kizayuni na vibaraka wao, bali muhimu zaidi ya hilo ni imani, irada, umoja na muqawama wa watu wake.

Kongamano la kimataifa la kuwaenzi mashahidi wa Ulimwengu wa Kiislamu na Siku ya Shahidi linalofanyika mjini Mash-had linahudhuriwa na wageni 30 waalikwa kutoka Iraq, Lebanon, Syria, Pakistan, Tunisia na Bosnia Herzegovina, jamaa 300 wa familia adhimu za mashahidi wa Iran pamoja na washiriki 400 kutoka mkoa wa Khorasan Razavi.../