Rouhani: Ushirikiano wa Iran, Russia unaweza kuleta usalama kieneo na kimataifa
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uhusiano wa Tehran na Moscow unazidi kustawi na kuongeza kuwa, Iran inakaribisha kuimarishwa uhusiano wa kina na nchi jirani ikiwa ni pamoja na Russia.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo Jumatatu usiku wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Russia Dimitry Medvedev mjini Moscow na kuongeza kuwa: "Nina matumaini kuwa safari hii itashuhudia matukio mapya katika mkondo wa kuimarisha uhusiano wa pamoja katika seta za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na masuala ya kimataifa."
Rais wa Iran ameashiria ushirikiano wa Tehran na Moscow katika masuala ya kieneo na kimataifa na kusema hakuna shaka uhsirikiano huu utakuwa na taathira chanya katika kuleta uthabaiti na usalama kieneo na kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Russia Dimitry Medvedev awali ametoa salamu za heri na fanaka za mwaka mpya wa Hijria Shamsia kwa rais na taifa la Iran na kusema: "Russia ina azma ya kuimarisha uhusiano wa pande zote na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."
Waziri Mkuu wa Ruusia ameitaja safari ya Rais wa Iran mjini Moscow kuwa muhimu na kuongeza kuwa, katika hali ya hivi sasa kuna mazingira mazuri katika uhusiano mzuri baina ya nchi hizi mbili. Amesema hakuna shaka kuwa safari ya Rouhani itakuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha uhusiano wa Tehran na Moscow.
Rais Hassan Rouhani jana jioni aliwasili Russia kufuatia mwaliko rasmi wa rais wa nchi hiyo Vladimir Putin. Marais hao wawili leo watafanya mazungumzo katika Ikulu ya Kremlin kwa lengo la kujadili uhusiano wa nchi mbili na pia matukio ya kieneo na kimataifa.