Iraq yasisitizia umuhimu wa kuwa na uhusiano mzuri na Iran
Spika wa Bunge la Iraq amesema kuna haja ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili kati ya nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Salim al-Jabouri, aliyasema hayo katika mazungumzo yake na Balozi wa Iran mjini Baghdad anayeondoka, Hassan Danaeifar, na kuongeza kuwa, nchi mbili hizi zina uhusiano mpana wa jadi na wa kijirani.
Spika wa Bunge la Iraq ameongeza kuwa, kuna haja ya kubadili maingiliano na misimamo yenye kufanana kati ya Tehran na Baghdad na kuipeleka katika hatua nyingine yenye maslahi ya pande mbili.
Kwa upande wake, Balozi wa Iran mjini Baghdad anayeondoka, Hassan Danaeifar amesisitiza kuwa, mabunge ya nchi mbili hizi yana nafasi kubwa na ya kipekee ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili.
Haya yanajiri katika hali ambayo, siku chache zilizopita, Ibrahim al Jaafari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq alisema kuwa nchi yake haiwezi kuiruhusu Marekani kuweka kambi zake za kijeshi katika ardhi ya nchi hiyo.
Iran na Iraq zimekuwa na uhusiano mzuri tokea tangu mwaka 2003, baada ya kuondolewa madarakani dikteta wa nchi hiyo ya Kiarabu, Saddam Hussein.