Iran yatoa jibu kwa uropokaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema uuzaji silaha kwa wavamizi kwa ajili ya kuulia watu wasio na hatia katika eneo hili na hasa katika uvamizi usio na mlingano na ulio dhidi ya ubinadamu uliofanywa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen hauwiyani na madai yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza.
Bahram Qassemi ameyasema hayo mapema leo kujibu madai ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May akiwa nchini Saudia ya kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inavuruga uthabiti katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema inasikitisha kwamba hii si mara ya kwanza ambapo Waziri Mkuu wa Uingereza anafadhilisha uongo kuliko ukweli.
Qassemi amebainisha kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza amefumbia macho historia ya mabadiliko na matukio ya miongo ya karibuni katika eneo na hivyo kwa kughafilika au kwa makusudi anasahau kwamba sehemu kubwa ya hali mbaya, kukosekana uthabiti na kubaki nyuma kiustawi eneo la Mashariki ya Kati vimetokana na siasa za kikoloni, kupenda kujitanua na uonevu uliofanywa na dola la kikoloni la Uingereza na waitifaki wake katika uvamizi na uchokozi liliofanya na katika kuwasha moto wa vita ndani ya nchi za eneo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa tuhuma zisizo na msingi za Theresa May zinatolewa katika hali ambayo hakuna asiyejua mchango muhimu wa Iran katika kusaidia kurejesha amani, uthabiti na usalama katika nchi zilizovamiwa na magaidi na ambazo zimeomba msaada na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Qassemi amemalizia kwa kusisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali matamshi ya aina hiyo yanayotolewa kwa madhumuni ya kuziridhisha baadhi ya nchi za eneo na kutafuta uungaji mkono wao wa kifedha, na inatarajia kuwa kwa kuelewa uhalisia wa mambo na kwa kutumia tajiriba na uzoefu mkubwa waliopata katika eneo la Ghuba ya Uajemi katika zama zilizopita, viongozi wa Uingereza watarekebisha misimamo yao potofu.../