Iran: Makombora yetu hayana uhusiano wowote na JCPOA
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amesema hatua ya Jamhuri ya Kiislamu kufanyia majaribio makombora yake haina mfungamano wowote na makubaliano ya nyuklia ya Vienna.
Bahram Qassemi amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kujiimarisha kiulinzi na kwamba hatua ya nchi hii kuimarisha mfumo wake wa makombora haina uhusiano wowote na makubaliano hayo yaliyofikiwa Julai mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa Januari mwaka jana 2016.
Matamshi ya Msemaji wa Wizara ya mambo ya Nje ya Iran ni radiamali kwa taarifa ya Kundi la Nchi 7 Zilizostawi Kiviwanda G7, iliyodai kuwa kitendo cha Tehran kuyafanyia majaribio makombora yake kinakinzana na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Hii ni katika hali ambayo, mwezi Februari mwaka huu, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwa mara nyingine tena ulitoa ripoti ya kuthibitisha kuwa Iran imeheshimu kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Mwezi mmoja kabla ya hapo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia lilitangaza katika kikao chake kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza majukumu yake yote kuhusu makubaliano ya nyuklia kati ya Tehran na kundi la 5+1.