Zoezi la kuwachuja wagombea urais Iran laanza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27860-zoezi_la_kuwachuja_wagombea_urais_iran_laanza
Zoezi la kuwachuja waliojiandikisha kugombea awamu ya 12 ya urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limeanza leo Jumapili na matokeo yanatazamiwa kutangazwa katika kipindi cha siku tano zijazo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 16, 2017 11:33 UTC
  • Zoezi la kuwachuja wagombea urais Iran laanza

Zoezi la kuwachuja waliojiandikisha kugombea awamu ya 12 ya urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limeanza leo Jumapili na matokeo yanatazamiwa kutangazwa katika kipindi cha siku tano zijazo.

Zoezi hilo la kuwachuja watu waliojiandikisha kugombea urais linafanywa na Baraza la Kulinda Katiba ambalo pia lina jukumu la kusimamia uchaguzi. Akizungumza na waandishi habari msemaji wa baraza hilo Abbas Ali Kadkhodaei amesema baraza hilo limeanza kazi yake na kuongeza kuwa, katiba inaruhusu zoezi hilo kuongezwa kwa muda wa siku zingine tano.

Uandikishaji wagombea urais ulimalizika jana Jumamosi ambapo watu 1,636, wakiwemo wanawake 137, walijiandikisha kugombea urais. Kampeni za uchaguzi wa rais zinatazamiwa kuanza rasmi wiki mbili kabla ya  siku ya kupiga kura mnamo Mei 19.

Sanduku la kupigia kura nchini Iran

Mbali na uchaguzi wa rais, siku hiyo pia kutafanyika uchaguzi wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji. Weledi wa mambo wanatabiri kuwa uchaguzi huo utakuwa na idadi kubwa ya wapiga kura hasa baada ya Rais Hassan Rouhani kutangaza nia yake ya kutetea kiti hicho. Kadkhodaei ametabiri kuwa idadi kubwa ya waliojisajili kugombea urais hawatapitishwa kwani katiba imeweka vigezo vya anayepaswa kushika wadhifa huo muhimu.